Swali: Mimi ni mwanamke mzee na kipofu. Nina kikosi cha watoto wadogo na umri wao ni wenye kukaribiana. Daima huhisi unyevu unaotokana na mkojo wao kwenye nguo zangu na kwenye magodoro yaliyoko nyumbani. Wakati fulani huhisi na nikaosha na wakati mwingine nahisi jambo hilo baada ya kumaliza kuswali. Sina ambaye anaweza kunisaidia kuyasafisha. Niswali vipi?  Je, inafaa kwangu kujengea juu ya yakini?

Jibu: Ni lazima kwako pale tu utapojua kitu katika najisi basi ukioshe kabla ya kuswali. Ni mamoja najisi hiyo iko kwenye kitu katika nguo zao au kwenye mwili wako. Ukiswali na usijue isipokuwa baada ya kumaliza kuswali basi hulazimiki kuirudia swalah yako kutokana na maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Allaah (Subhaanah) amesema:

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا

“Ee Mola wetu! Usituchukulie pale tutaposahau au tukikosea.”[1]

Pia imesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba Allaah ameikubali du´aa hii.

Vilevile imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba siku moja alikuwa akiswali kwenye viatu vyake. Jibriyl (´alayhis-Salaam) akamweleza kwamba vina uchafu ambapo akavivua na akakamilisha swalah yake.

Kuhusu najisi ilioko juu ya ardhi au godoro ni lazima sehemu yake kubwa kuimwagilia maji na hivyo inasafika kwa njia hiyo. Kwa sababu imethibiti kutoka kwa Abu Hurayrah na Anas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kwamba kuna mbedui mmoja alikojoa ndani ya msikiti ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaamrisha kumwagia juu ya mkojo wake ndoo ya maji.

Imewekwa katika Shari´ah kuwataka msaada wale wanamme waaminifu ambao ni Mahaarim zako au wanawake kuhusu kutambua ni wapi ulipo mkojo kwenye kitanda ili wamwagie juu yake maji.

[1] 02:286

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/400)
  • Imechapishwa: 27/09/2021