Swali: Ulipokuwa ukifasiri maneno Yake (Ta´ala):

وَالَّذِينَ لَا يَشْهَدُونَ الزُّورَ

“Wale ambao hawashuhudii uongo.”[1]

umezungumzia kuhusu. Je, kuhudhuria katika sherehe ya mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kunaingia katika uongo huu? Je, mtu akialikwa ima kuja kuhudhuria au kuja kutoa muhadhara katika mfano wa sherehe kama hizi ahudhurie au hapana?

Jibu: Kusherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni jambo lisilotambulika kutoka kwa as-Salaf as-Swaalih; halikufanywa na makhaliyfah waongofu, Maswahabah, wale waliowafuata kwa wema wala maimamu wa waislamu baada yao. Je, hivi kweli sisi ni wenye kumuadhimisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zaidi kuliko watu hawa? Hapana. Je, sisi ni wenye kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zaidi kuliko watu hawa? Hapana. Mambo yakishakuwa ni hivo basi lililo wajibu kwetu ni sisi kuigiliza mwenendo wao na wala tusisimamishe mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sababu ni Bid´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maulidi wapi na wapi? Ni kwa nini hajasherehekea mazazi yake? Wako wapi makhaliyfah waongofu? Wako wapi Maswahabah? Je, wao hawayajui haya, walificha haki au waliifanyia jeuri? Yote haya hayayumkiniki. Hapana shaka kwamba wengi katika wale wanaosherehekea mazazi haya wanayafanya kwa nia nzuri. Wanafanya hivo ima kwa sababu ya kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au kwa kuwaiga manaswara ambao wanasherehekea mazazi ya ´Iysaa mwana wa Maryam (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo na wao wanaona kuwa wana haki zaidi ya kufanya hivo. Lakini yote haya ni kufikiria kubaya. Kwa sababu kila ambavyo mtu atakuwa ni mwenye kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndivo atakuwa ni mwenye kujitenga mbali zaidi na Bid´ah. Kwa sababu mtu huyu akizusha na akasema kuwa anajikurubisha kwa Allaah kwa Bid´ah hiyo, basi tunasema kuwa ameingiza katika dini ya Allaah yasiyokuwemo na ametangulia mbele ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ikiwa atasema kuwa anasherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kiada, basi tutamuuliza kama ada zinasimamishwa kwa kujengea ada au kwa kujengea Shari´ah? Ni kwa kujengea Shari´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofika al-Madiynah na akawakuta wanasherehekea sikukuu mbili kwa sababu ya kumbukumbu ya ushindi, akawakataza juu ya hilo na akawaambia:

“Allaah amekubadilishieni bora zaidi kuliko hizo mbili; ´Iyd-ul-Adhwhaa na ´Iyd-ul-Fitwr.”

Ni vipi mtasherekea? Wakisema kwamba wanasherehekea kwa sababu ya kuhuisha kumkumbuka Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Basi tutawajibu kwa kusema:

Mosi: Haikusihi kuwa kuzaliwa kwake kulikuwa tarehe kumi na mbili.

Pili: Kungelisihi basi kumkumbuka Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni jambo linatakiwa kuwa kila siku. Je, waislamu kila siku si wanasema ´nashuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah` katika adhaana? Ndio. Bali mtu katika kila swalah anaposoma Tashahhud anasema:

السلام عليك أيها النبي ورحمة الله وبركاته، السلام علينا وعلى عباد الله الصالحين، أشهد أن لا إله إلا الله وأشهد أن محمداً عبده ورسوله

“Amani ya Allaah iwe juu yako, ee Nabii, na rehema na baraka za Allaah. Amani ya Allaah iwe juu yetu na juu ya waja wa Allaah wema. Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake.”

Muumini anamkumbuka siku zote na sio tu katika usiku maalum. Lakini kwa vile watu wengi hawajui mfano wa jambo kama hili na hawajui ukhatari wa Bid´ah ndio maana wameendelea. Lakini sifa njema zote kamilifu zimwendee Allaah nataraji kwamba watu wengi hii leo, na khaswakhaswa vijana, wamejua kuwa Bid´ah hii haina msingi wala uhakika wowote.

[1] 25:72

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (66) http://binothaimeen.net/content/1478
  • Imechapishwa: 30/10/2019