Kumtolea salamu ambaye sina uhakika kama ni muislamu

Swali: Ni ipi hukumu ya kumtolea salamu mtu ambaye sijui kama ni muislamu au kafiri? Pamoja na kuzingatia ya kwamba iwapo nitaacha kumtolea salamu basi inaweza kupelekea katika chuki na kuwa mbali na Uislamu?

Jibu: Hili linarudi katika jamii. Ikiwa wengi katika jamii sio waislamu, basi hapa usitoe salamu kwa kujengea ule wingi. Kwa sababu wengi wanapewa hukumu ya wote pale ambapo mtu anakuwa hana ujuzi. Ama ikiwa wengi walioko katika jamii ni waislamu atoe salamu. Tukikadiria kuwa amemtolea salamu ambaye si muislamu, basi hana juu yake kitu. Hakujua. Jengine ni kwamba huenda kule kumtolea salamu ambaye si muislamu ikawa ni sababu ya kuingia kwake katika Uislamu na kuuelekea Uislamu.

Kwa kifupi ni kwamba ikiwa wengi walioko katika jamii ni waislamu basi atoe salamu. Ikiwa wengi walioko katika jamii sio waislamu asitoe salamu. Akiwa na mashaka na wasiwasi atoe salamu. Kwa sababu kimsingi ni kwamba imewekwa katika Shari´ah kutoa salamu.

Makusudio yangu ya “jamii” kwa mfano ikiwa ni wafanyakazi na wengi katika wafanyakazi ni waislamu, basi awatolee salamu. Lakini wengi katika wafanyakazi wakiwa sio waislamu, asiwatolee salamu. Lakini jamii iliobaki ikiwa hawako namna hii, awatolee salamu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (47) http://binothaimeen.net/content/1073
  • Imechapishwa: 24/03/2019