Kufunga Rajab yote, Sha´baan yote na Ramadhaan yote


Swali: Nawaona watu wanadumu kufunga Rajab na Sha´baan kisha wanafuatisha Ramadhaan bila kukatikiza swawm katika muda wote huu. Je, kumethibiti Hadiyht juu ya hilo na kama ndio ni ipi?

Jibu: Haikusihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba alifunga mwezi wa Rajab kamili wala mwezi wa Sha´baan kamili. Wala hilo halikuthibiti kutoka kwa yeyote katika Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum).  Hakuna mwezi wowote ambao ilithibiti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifunga mwezi kamili isipokuwa tu Ramadhaan. Imethibiti kuwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifunga mapka tunasema kuwa hatofungua na akiacha kufunga mpaka tunasema hatofunga. Hatujapatapo kumuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akifunga mwezi wowote kamili isipokuwa Ramadhaan. Hatujamuona mwezi wowote akifunga sana isipokuwa Sha´baan.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hajapatapo kamwe kufunga mwez wowote kamili isipokuwa Ramadhaan. Alikuwa akifunga mpaka anasema mwenye kusema “naapa kwa Allaah ya kwamba hatoacha kufunga” na anaacha kufunga mpaka anasema mwenye kusema “naapa kwa Allaah ya kwa kwamba hatofunga”.

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Kwa hivyo mtu kujitolea kufunga Rajab yote na Sha´baan yote ni kwenda kinyume na mwongozo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akionelea kuwa ni sunnah kufanya hivo basi hiyo itakuwa ni Bid´ah iliyozuliwa. Imethibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu hii, basi atarudishiwa mwenyewe.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.alifta.net/Fatawa/FatawaChapters.aspx?languagename=ar&View=Page&PageID=346&PageNo=1&BookID=12
  • Imechapishwa: 22/03/2018