Ulazima wa kitoka nyumba kwa mwanamke aliyeachwa

Udhahiri wa maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

وَمَتِّعُوهُنَّ

“Wapeni kiliwazo… “[1]

pamoja na:

وَلِلْمُطَلَّقَاتِ مَتَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ ۖ حَقًّا عَلَى الْمُتَّقِينَ

“Wanawake waliotalikiwa wapewe kitoka nyumba kwa mujibu wa Shari´ah. Ni haki kwa wale wenye kumcha Allaah.”[2]

yanapelekea ulazima wa kumpa kitoka nyumba yule mwanamke anayeachwa. Maalik na wengine wenye kuonelea kama yeye wanaona kuwa si lazima kutoa kitoka nyumba kabisa. Baadhi ya Maalikiyyah wametumia hoja kwa maneno ya Allaah (Ta´ala) yanayosema:

حَقًّا عَلَى الْمُحْسِنِينَ

“Ni haki kwa watenda wema.”[3]

na:

حَقًّا عَلَى الْمُتَّقِينَ

“Ni haki kwa wale wenye kumcha Allaah.”

Wamesema kuwa endapo kitoka nyumba kingelikuwa ni lazima basi kingelimuwajibikia kila mmoja na kungebainishwa kiwango ambacho ni cha lazima. Lakini dalili yao haileti tofauti yoyote. Kwa sababu kitoka nyumba kuwa ni haki kwa wale watendao wema na wale wenye kumcha Allaah kunatilia nguvu zaidi ulazima wake. Hakuna yeyote ambaye ana haki ya kusema kuwa si mwenye kumcha Allaah, kwa sababu kila mtu analazima kumcha Allaah. al-Qurtwuubiy amesema:

“Kitoka nyumba kuwa ni haki juu ya wale wenye kumcha Allaah kunatilia nguvu juu ya uwajibu wake, kwa sababu kila mmoja ana ulazima wa kumcha Allaah na kujiepusha na shirki na dhambi. Kwani Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu Qur-aan:

ذَلِكَ الْكِتَابُ لاَ رَيْبَ فِيهِ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ

“HICHI ni Kitabu – kisichokuwa na shaka – ni uongofu kwa wamchao Allaah.”[4]

Kusema kwamba endapo kitoka nyumba kingelikuwa ni lazima basi kungebainishwa kiwango chake ni hoja dhaifu. Kwani ni lazima kuwahudumia wake na jamaa ingawa hakukutajwa kiwango maalum cha wajibu.

[1] 02:236

[2] 02:241

[3] 02:241

[4] 02:02

  • Mhusika: Imaam Muhammad al-Amiyn ash-Shanqiytwiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Adhwaa’-ul-Bayaan (5/87)