Swali: Kuna ndugu mmoja amezungumza kuhusu usengenyi. Ameonya juu ya usengenyi na yale yanayofanywa na Muhammad al-Mas´ariy pindi anapoeneza majarida haya ya batili. Ndipo akasimama bwana mmoja na kumwambia kwamba kitendo ambacho yeye mwenyewe anafanya ni kumsengenya mtu huyo. Je, haya ni kweli? Je, ni kweli yale yanayosemwa juu yako kwamba umesema kuwa bwana huyu al-Mas´ariy hana heshima na hivyo inafaa kumsengenya? Hivo ndivo tumevosikia na tunataraji uthibitisho.

Jibu: Kuhusu ambaye anatahadharisha juu ya usengenyi na majarida ya bwana huyo uliyemtaja, hapana shaka kwamba ni sahihi. Makatazo ya usengenyi yametajwa ndani ya Kitabu cha Allaah:

وَلَا تَجَسَّسُوا وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ

”Wala wasisengenyane baadhi yenu wengine. Je, anapenda mmoja wenu kula nyama ya nduguye aliyekufa; basi mmelichukia hilo?”[1]

Anayo haki.

Kuhusu mtu ambaye amesema kuwa kumtaja mtu huyu kunaingia pia katika kusengenya, sio usengenyi. Bali ni nasaha. Kumtaja mtu kwa mambo anayoyachukia kwa lengo la kuwanasihi waislamu ni katika nasaha na jambo jema. Pindi Faatwimah bint Qays alipokuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwomba ushauri juu ya Mu´aawiyah, Abu Jahm na Usaamah bin Zayd waliokuwa wamemposa na anataka kujua amchague nani, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia:

”Ama kuhusu Mu´aawiyah, ni masikini hana pesa yoyote. Ama Abu Jahm, ni mwenye kuwapiga wanawake. Olewa na Usaamah.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawataja mabwana hawa wawili kwa njia wanayoichukia. Kwa nini alifanya hivo? Kwa ajili ya kutoa nasaha.

Ikiwa kumtaja kwetu bwana huyu anayeeneza vurugu kati ya watu na anataja kasoro za wanachuoni na za viongozi  ni kwa lengo la kutoa nasaha na kuwatahadharisha watu kutokamana naye, basi ni jambo zuri. Ni njia moja wapo ya mtu kujikurubisha mbele ya Mola wake.

Yule anayekataza jambo hili, bi maana kumtahadharisha bwana huyu, ni mwenye kukataza jambo jema na nasaha.

Mimi naona kuwa bwana huyu aachwe. Asiwe ni sababu ya mizozo kati ya vijana na watu wengine. Nadhani kwamba asipotajwa kwa wingi, basi atazimia kwa idhini ya Allaah:

إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الظَّالِمُونَ

“Hakika madhalimu hawatofaulu.”[2]

إِنَّ اللَّـهَ لَا يُصْلِحُ عَمَلَ الْمُفْسِدِينَ

”Hakika Allaah hatengenezi matendo ya waharibifu.”[3]

Swali: Wanaeneza majarida haya…

Jibu: Watapata malipo yao.

Swali: Je, ni kweli kwamba umesema kuwa bwana huyu hana heshima na hivyo inafaa kumsengenya?

Jibu: Kamwe. Mimi nina desturi ya kumtomtaja mtu kwa jina lake. Ndio maana utaona katika jawabu langu hili sipendi kumtaja jina lake. Bora ni kuyafungamanisha mambo kwa sifa kuliko kuyafungamanisha na watu. Ukimtaja mtu pengine mtu huyo akaja kutubia na akarejea kwa Allaah, maneno yako juu yake yanakuwa ni yenye kubaki mpaka siku ya Qiyaamah. Lakini ukimtaja kwa sifa zake, basi yanakuwa ni yenye kumgusa yeye na wengine na kama Allaah atataka kumwongoza, basi ataachwa kukosolewa. Kwa ajili hiyo ndio maana nasema kuwa ni lazima kutahadharisha juu ya kila mtu anayeeneza mipasuko na kasoro.

[1] 49:12

[2] 06:21

[3] 10:81

  • Mhusika: Imâm Muhammad bin Sâlih bin ´Uthaymîn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (98 B) Tarehe: 1416-02-08/1995-06-07 http://www.youtube.com/watch?v=Mo7ECe5CJw0
  • Imechapishwa: 06/12/2020