Ibn ´Uthaymiyn kuhusu kuigawanya swalah ya usiku kati ya Tarawiyh na Tahajjud

Swali: Vipi kuhusu mwenye kuswali na imamu wa kwanza swalah ya Tarawiyh kisha akaondoka zake na kusema kuwa ameandikiwa thawabu za kuswali usiku mzima kwa dalili ya Hadiyth:

“Atakayesimama pamoja na imamu mpaka akamaliza basi anaandikiwa kuwa ameswali usiku mzima.”

na kwamba ameanza na imamu na kumaliza naye?

Jibu: Kuhusu maneno yake:

“Atakayesimama pamoja na imamu mpaka akamaliza basi anaandikiwa kuwa ameswali usiku mzima.”

ni Hadiyth Swahiyh ambayo imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi Maswahabah walipomuomba waswali usiku uliyobaki baada ya (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kukatisha swalah katikati ya usiku. Ndipo wakasema:

“Ee Mtume wa Allaah! Laiti tungekesha usiku uliyobaki.” Ndipo akasema: “Hakika yule atakayesimama pamoja na imamu mpaka akamaliza basi anaandikiwa kuwa ameswali usiku mzima.”

Lakini maimamu wawili katika msikiti mmoja wanazingatiwa kila mmoja yuko kivyake au kila mmoja ni naibu wa mwengine? Kilicho dhahiri ni tafsiri hii ya pili; kila mmoja ni naibu anayechukua nafasi ya mwengine.

Kujengea juu ya hili ikiwa kuna msikiti ambao wanaswalisha maimamu wawili basi maimamu hawa wawili wanazingatiwa wako katika ngazi ya imamu mmoja. Kwa hivyo mtu anatakiwa kubaki mpaka amalize yule imamu wa pili. Tunatambua kuwa yule imamu wa pili ni mwenye kukamilisha swalah ya yule wa kwanza.

Kutokana na hili tunawanasihi ndugu zetu wawafuate maimamu hapa katika msikiti Mtakatifu mpaka wamalize kabisa. Japokuwa kuna baadhi ya ndugu wanaoenda zao baada ya kuswali Rak´ah kumi na moja na wanasema kuwa hii ndio idadi ya swalah alizokuwa akiswali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Sisi tunakubaliana nao ya kwamba hiyo ndio idadi aliyokuwa akiswali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ndio bora kukomeka katika idadi hiyo. Hakuna yeyote anayetilia mashaka hili. Lakini mimi binafsi naonelea kuwa hakuna makatazo ya kuzidisha, sio kwa msingi wa kupuuzia idadi iliyochaguliwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini ni kwa msingi wa kwamba hii ni kheri moja wapo ambayo Shari´ah imepanua. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa kuhusu swalah ya usiku ambapo akasema:

“Ni mbili mbili. Atapochelea mmoja wenu kuingia kwa asubuhi basi aswali moja ili kuwitirisha aliyoswali.”

Ikiwa jambo hili ni miongoni mwa mambo ambayo Ijtihaad inakubalika, basi lililo bora kwa mtu ni yeye kutotenga mkusanyiko. Bali anachotakiwa ni kufuata mkusanyiko. Pindi ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) aliposwali kikamilifu Minaa basi Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walikemea kitendo hicho. Lakini pamoja na hivyo walikuwa wakiswali nyuma yake Rak´ah nne na hivyo wakizidisha Rak´ah mbili katika swalah ambayo hakuzidishwi Rak´ah mbili. Wanafanya yote haya kwa sababu ya kuafikiana na mkusanyiko, kuleta umoja na kutofarikiana. Umoja ni jambo muhimu sana. Mmoja wenu asifuate mrengo wake aliopwekeka nao kutokamana na mkusanyiko na akaupasua Ummah na huku akitazama ni wapi walio pamoja naye na ni wepi wasiokuwa pamoja naye. Hili ni kosa.

Kujengea juu ya hili maadamu jambo hili ni pana na hakuna makatazo ya Kishari´ah basi hakika kuafikiana na mkusanyiko hakuleti picha ya bughudha wala vifundo. Midhali jambo hili ni pana na katika nafais ya mbele kumepokelewa kutoka kwa as-Salaf as-Swaalih  yanayofahamisha hivo, kama alivyosema Imaam Ahmad na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahumaa Allaah), basi yatutoshe yale yaliyowatosha Salaf. Kuna katika Salaf waliotangulia katika hili. Hivyo basi haitakikani kwenda kinyume. Mimi nakariri kulingania katika umoja na kutotafautiana katika jambo ambalo Ijtihaad inakubalika.

Lakini utatizi uliopo ni maamuma wafanye nini kukiwepo Witr mara mbili katika usiku mmoja? Ikiwa unataka kuswali Tahajjud na imamu wa pili, imamu wa kwanza atakapomaliza kuswali Witr basi ongeza Rak´ah moja ili ziwe mbili. Ikiwa hutaki kuswali Tahajjud mwishoni mwa usiku na imamu, swali Witr na yule imamu wa kwanza. Baada ya hapo ukiwezeshwa kuswali Tahajjud, basi Witr yako ifanye shafaa´ na yule imamu wa pili.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (14/206-208)
  • Imechapishwa: 18/06/2017