Ibn Baaz kuhusu “Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” ya al-Albaaniy

Swali: Unasemaje kuhusu “Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” ya Shaykh al-Albaaniy?

Jibu: Vitabu vya al-Albaaniy ni vizuri na vyenye faida. Ni katika ndugu zetu wazuri na ambao wana ´Aqiydah nzuri. Vitabu vyake “Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah” na “Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” vyote ni vyenye faida. Lakini havisalimiki kutokamana na ukosolewaji hapa na pale, kila mmoja yanakubaliwa na kukataliwa maneno yake. Si yeye wala mwanachuoni mwingine yeyote hakuna ambaye amekingwa na kukosea. Anaweza kupwekeka kwa jambo katika “Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” na katika “Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah”. Lakini hilo ni jambo ambalo linaweza kuzinduliwa na wanachuoni na watambuzi ambao wana elimu kuhusu Hadiyth, njia na wapokezi wake. Yeye ni Mujtahid na ni mwenye kupatia kwa ujumla. Lakini haina maana kuwa ni mwenye kupatia katika kila alisemalo na kwamba hakosei. Hilo ni jambo linaweza kumtokea. Limemtokea. Sote tunakosea. Kila mtu anakosea, hata wanachuoni wakubwa walioishi kabla yake. Haina maana kwamba ni mwenye kukubaliwa kila alisemalo. Anaweza kukosea. Mwanafunzi anatakiwa kuzindukana, kumrejea na amtilie umuhimu. Hata hivyo ni katika bora ya wanachuoni wa zama hizi. Allaah amuwafikishe na amzidishie kheri.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/21084
  • Imechapishwa: 21/08/2020