Ibn Baaz kuhusu kusherehekea krismasi na mwaka mpya

Swali: Baadhi ya waislamu wanashirikiana na wakristo katika sikukuu ya krismasi.

Jibu: Haijuzu kwa muislamu wa kiume wala muislamu wa kike kushirikiana na manaswara, mayahudi na makafiri wengine kasika sikukuu zao. Bali ni lazima kuacha kitendo hicho. Kwa sababu mwenye kujifananisha na watu basi yeye ni katika wao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametutahadharisha kujifananisha nao na kujipamba kwa tabia zao. Ni lazima kwa muumini wa kiume na muumini wa kike kutahadhari kutokamana na hilo. Asiwasaidie kutekeleza sikukuu hizi kwa kitu chochote. Kwa sababu ni sikukuu zinazokwenda kinyume na Shari´ah ya Allaah na zinafanywa na maadui wa Allaah. Kwa hiyo haijuzu kushiriki ndani yake wala kusaidiana na watu wake. Wala haifai kuwasaidia kwa kitu chochote; si kwa chai, wala kahawa wala kitu chochote kama vile vyombo na mfano wake. Isitoshe Allaah (Subhaanah) amesema:

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ

“Saidizaneni katika wema na kumcha Allaah na wala msisaidizane katika dhambi na uadui.” (05:02)

Kushirikiana pamoja na makafiri katika sikukuu zao ni aina fulani ya kusaidizana katika madhambi na uadui.

Kwa hivyo ni lazima kwa kila muislamu wa kiume na muislamu wa kike kuacha kitendo hicho.

Mtu hatakiwi kudanganyika na matendo ya watu. Ni lazima aitazame Shari´ah ya Uislamu na yale yaliyomo ndani yake. Vilevile anatakiwa kutekeleza amri ya Allaah na Mtume Wake na asitazame mambo ya watu. Kwani watu wengi wanapuuza yale ambayo Allaah ameyaweka katika Shari´ah. Allaah (´Azza wa Jall) amesema ndani ya Kitabu Chake kitukufu:

وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ

“Ukiwatii wengi walioko ulimwenguni, basi watakupoteza kutokamana na njia ya Allaah.” (06:116)

وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ

“Wengi wa watu hawatoamini ijapokuwa utalitilia hima.” (12:103)

Sikukuu zinazokwenda kinyume na Shari´ah haijuzu kuzifanya hata kama watu watazifanya. Muumini anayapima matendo na maneno yake na vilevile anapima maneno na matendo ya watu wengine juu ya Qur-aan na Sunnah. Kile kinachokwenda sambamba navyo au kimoja wapo ndio chenye kukubaliwa ijapokuwa watu watakiacha. Na kile kinachokwenda kinyume navyo ni chenye kurudishwa ijapokuwa watu watakifanya.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´ Fataawaa wa Maqaalaat Mutanawwi´ah (6/405) https://binbaz.org.sa/fatwas/29103/%D8%AD%D9%83%D9%85-%D9%85%D8%B4%D8%A7%D8%B1%D9%83%D8%A9-%D8%A7%D9%84%D9%85%D8%B3%D9%84%D9%85%D9%8A%D9%86-%D9%84%D9%84%D9%85%D8%B3%D9%8A%D8%AD%D9%8A%D9%8A%D9%86-%D9%81%D9%8A-%D8%B9%D9%8A%D8%AF-%D8%A7%D9%84%D9%85%D9%8A%D9%84%D8%A7%D8%AF
  • Imechapishwa: 18/12/2019