Hii ni dalili tosha kuonesha namna ya uharibifu wa ISIS

Hili ni swali kutoka Libya ambapo kunaulizwa juu ya qadhiya ya ya Sirte na mapambano yao dhidi ya ISIS.

Kwanza wanauliza hukumu ya kupambana na pote hili.

Pili wanauliza kuhusu kuwasaidia wengine na ndugu zao walioko Sirte.

Tatu wanauliza wapigane vita na kina nani.

Mosi ni kwamba ISIS kundi la kijambazi la Khawaarij. Sijui kama kuna kundi katika Khawaarij ambalo lina madhara juu ya Uislamu na waislamu kama kundi hili. Ni kundi la Khawaarij la kijambazi. Muislamu asidanganyike na yale wanayoyaona kwao. Uhalisia ni kwamba wako mbali kabisa na Uislamu. Matendo yao hayana lolote kuhusiana na Uislamu. Hayajuzu kuyanasibisha na Uislamu. Bali ni wajibu kwa kila muislamu ambaye ana elimu, maarifa na uwezo wa kupambanua kundi hili awanasihi waislamu na kutahadharisha nao. Ni kundi la kifisadi na la jinai linaloiharibu miji ya Kiislamu. Wameharibu ´Iraaq, Syria, Misri, Libya, Tunisia, Mali, kaskazini magharibi mwa Mauritania, kusini mwa Algeria, Yemen na huku kwetu Saudi Arabia.

Tunamuomba Allaah awaponde, awatokomeze na afanye waislamu wawashinde, awadhalilishe na awafedheheshe.

Pili wakivamia majumba yenu wapigeni vita. Andaeni uongozi ambao mtajiunga chini yake na mpambane nao. Wakipata mamlaka juu yenu basi watakutieni adabu kwelikweli. Hawawawekei wailsamu heshima yoyote. Wanawachukulia waislamu usahali zaidi ya nzi na wadudu wachungu. Mmejionea wenyewe namna ambavyo wanawaunguza na moto wapinzani wao.

Lakini hata hivyo kitu ambacho kinawaliwaza waislamu na waumini ni yale mapokezi Swahiyh ya Mtume juu yao na mababu zao:

“Ni mijibwa ya Motoni.”

“Ni wauliwa waovu kabisa waliouliwa chini ya mbingu.”

“Twuubaa kwa yule aliyewaua au kuuliwa nao.”

Bi maana Pepo.

“Yule mwenye kuwaua ana ujira.”

Kwa ajili hiyo ndio maana ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) aliwapiga vita Nahrawaan. Wengi katika Khawaarij hawa ni kama alivyosema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Katika zama za mwisho watajitokeza watu. Ni watu wenye meno yenye kuanza kuota na ni wapumbavu wa akili. Wanazungumza kwa maneno ya kiumbe aliye bora kabisa, wanatoka katika dini kama jinsi mshale unavyotoka katika upinde wake. Imani hazivuki koromeo zao. Waueni popote mtapokutana nao. Yule atakayewaua basi kwa hakika atalipwa ujira mkubwa siku ya Qiyaamah.”

Inatosha ya kwamba katika wao huwezi kupata mwanachuoni hata mmoja. Hawajinasibishi kwa mwanachuoni yeyote katika Ummah wa Kiislamu. Vivyo hivyo ndivyo walivyokuwa mababu zao. Pindi ´Abdullaah bin ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alipofika kwa ajili ya kujadiliana nao alisema:

“Nimekujieni kutoka kwa Maswahabah zake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na simuoni hata mmoja katika nyinyi.”

Bi maana mwenendo wao ni wenye kutofautiana na mwenendo wa Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

“Ummah wangu utatofautiana katika mapote sabini na tatu; yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Wakasema: “Ni kina nani hao, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni wale wenye kufuata yale ninayofuata mimi hii leo na Maswahabah zangu.” at-Tirmidhiy (2641).

Allaah amesema kuhusu Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum):

مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّـهَ عَلَيْهِ ۖ فَمِنْهُم مَّن قَضَىٰ نَحْبَهُ وَمِنْهُم مَّن يَنتَظِرُ ۖ وَمَا بَدَّلُوا تَبْدِيلًا

“Miongoni mwa Waumini, [wapo] wanaume wamesadikisha yale waliyomuahidi Allaah; basi miongoni mwao aliyetimiza nadhiri yake na miongoni mwao anayengojea na hawakubadilisha mabadiliko yoyote.” (33:23)

Wale waliojitolea maisha yao walikufa katika Uislamu na imani. Na ambao hawakufanya hivo Allaah amedhamini kuwa hawatozibadilisha imani zao. Hakuna yeyote katika Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa katika Khawaarij hawa. Hili tu linatolea ushuhuda kuonesha uharibifu wa madhehebu yao. Lau yangelikuwa ya kheri basi Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wangelikuwa kati yao. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Maswahabah zangu ni walinzi wa Ummah wangu. Pindi watapoondoka Maswahabah zangu basi Ummah wangu utafikwa na waliyoahidiwa.”

Lau kungelikuwa kheri yoyote katika watu hawa basi Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) wangelikuwa katika wao – lakini hakuna kheri yoyote katika wao. Hakuna Swahabah hata mmoja wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa katika wao au na wao. Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa bega kwa bega na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhum) pindi alipowapiga vita. Wale Maswahabah ambao hawakujaliwa kushiriki vita dhidi yao walijuta baadaye. Walisikitika kuona hawakuweza kushiriki katika kuwapiga vita mijibwa hii, mijibwa ya Motoni. Mtaona namna ambavyo watu hawa hawana mwanachuoni hata mmoja. Hakuna mwanachuoni hata mmoja ambao ni warithi wa Mitume yuko katika wao. Hii ni dalili tosha kuonesha ufisadi waliyomo.

  • Mhusika: ´Allaamah Muhammad bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://ar.miraath.net/fatwah/12009
  • Imechapishwa: 06/11/2016