Hedhi inayomjia mwanamke baada ya miaka khamsini

Swali: Ada ya mwezi inayomjia mwanamke anapofikisha miaka khamsini haizingatii na hivyo anatakiwa kuswali na kufunga?

Jibu: Wanazuoni wametofautiana katika jambo hilo. Miongoni mwao wako ambao wamefanya kikomo cha hedhi ni miaka khamsini na wengine wamefanya kuwa kikomo cha hedhi ni miaka sitini. Katika jambo hili hakuna dalili ya wazi. Isipokuwa yaliyothibiti kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:

“Mwanamke hahisi kitu tumboni mwake baada ya khamsini.”

Haya ameyasema kutokana na ijtihaad yake. Maoni ya sawa ni kwamba hedhi ikiendelea kumtoka na isibadilike, ijapo ni baada ya khamsini, basi anatakiwa kukaa. Kwa sababu hakuna dalili ya kikomo cha muda. Lakini ikivurugika baada ya khamsini na hali yake ikabadilika basi hiyo ni alama ya ukomaji na ni alama kuwa sio hedhi. Ikivurugika baada ya khamsini basi haizingatiwi kuwa ni hedhi na hiyo inakuwa ni dalili ya kumalizika kwake. Hapo ni pale ambapo mara inakuwa nyekundu, mara inakuwa njano, mara inakuwa rangi zambarau, mara inakuwa nyingi, mara inapungua, mara yaja na mara inapotea. Kwa msemo mwingine inavurugika. Kuna mwezi inakuja, mwezi mwingine haiji, mwezi mmoja siku tano, mwezi mwingine siku kumi, mwezi mwingine siku nane baada ya miaka khamsini. Mara inakuwa nyeusi, mara inakuwa nyekundu na kadhalika. Bi maana inabadilikabadilika. Hiyo ni dalili kuonyesha kuwa jambo lake limekwisha. Damu kama hiyo haizingatiwi. Damu kama hiyo inazingatiwa ni damu ya kawaida kama ilivyo damu ya ugonjwa. Ataswali na kufunga akiwa na damu hiyo baada ya kujihifadhi kwa pamba na mfano wake. Atatawadha kwa ajili ya kila swalah muda wa kuwa damu hiyo inamtoka pindi inapomvurugika na kuharibika baada ya miaka khamsini.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/4307/ما-حكم-من-تحيض-في-عمر-الخمسين
  • Imechapishwa: 15/06/2022