Nasaha kwa viongozi wa waislamu makusudio yake katika Hadiyth ni viongozi waliosimamia mambo yote kwa jumla. Kuhusiana na viongozi wa dini wana haki vilevile ya kupewa nasaha. Kuwanasihi wanachuoni ina maana ya kuwapenda kutokana na dini waliyomo na yale wanayowatumia watu katika elimu na kheri. Inatakiwa kuwanusuru kwa yale wanayoyasema katika mambo ya Shari´ah na yale wanayoyafikisha kutoka kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa), kuwatetea wao na heshima zao. Inatakiwa vilevile kuwapenda zaidi kuliko waumini wengine. Kwa sababu Allaah Amefungamanisha mapenzi kati ya waumini kwa Kusema:

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ

“Na waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki walinzi wao kwa wao.” (09:71)

Bi maana hupendana kati yao na kunusuriana. Ni jambo linalojulikana ya kwamba waumini wenye imani zilizo juu kabisa ni wanachuoni waliobobea katika elimu au kwa msemo mwingine ni wale wanachuoni wenye kuitendea kazi elimu yao. Allaah (Ta´ala) Amesema:

يَرْفَعِ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَالَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ دَرَجَاتٍ

“Allaah Atawainua wale walioamini miongoni mwenu na waliopewa elimu daraja za juu.” (48:11)

Nasaha kwa wanachuoni inatakiwa kuwapenda, kuwalindia heshima zao, kuchukua elimu wanayoitoa, kuwanasuru kwa yale wanayoinusru Shari´ah, kuzihifadhi nafasi zao na kueneza kwao elimu na dini. Zote hizi ni haki ambazo ni wajibu kwao [kufanyiwa]. Kwa kuwa wana nafasi kuu katika dini.

Wanachuoni wakitukanwa na wasipewe nasaha ambazo ni wajibu kwao kwa maana hii tuliyoitaja, hii ina maana ya kwamba haiba ya Shari´ah itadhoofika kwenye mioyo ya watu kwa sababu hayo yananukuu wanachuoni.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Arba´iyn an-Nawawiyyah, uk. 167
  • Imechapishwa: 17/05/2020