Funga Shawwaal jumatatu na alkhamisi ulipwe mara mbili

Swali: Je, mtu anapata thawabu za kufunga siku sita za Shawwaal ikiwa ana deni kabla ya kumaliza kulipa deni lake la Ramadhaan?

Jibu: Mtu halipwi thawabu za kufunga siku sita za Shawwaal ikiwa hajakamilisha Ramadhaan nzima. Kwa yule mwenye deni la Ramadhaan basi asifunge siku sita za Shawwaal mpaka kwanza akamilishe Ramadhaan nzima, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayefunga Ramadhaan kisha akaifuatishia siku sita za Shawwaal basi ni kama ambaye amefunga mwaka mzima.”

Kutokana na hili tunasema kumwambia yule mwenye deni kwanza aanze kufunga deni lake kisha ndio afunge siku sita za Shawwaal. Shawwaal ikimalizika kabla ya kuwahi kufunga hizo siku sita, basi thawabu zake zinapotea isipokuwa kama amechelewesha kwa udhuru. Mtu akijaaliwa kufunga siku sita hizo kila jumatatu na alkhamisi basi analipwa thawabu mara mbili kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika kila kitendo kinategemea na nia na kila mmoja atalipwa kutokana na vile alivyonuia.”[1]

[1] al-Bukhaariy (1) na Muslim (1907).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (20/18-19)
  • Imechapishwa: 06/06/2019