Hapa ndipo mtu atapata fadhilah za siku sita za Shawwaal

Swali: Je, kuna fadhilah yoyote ya kufunga siku sita za Shawwaal? Mtu afunge kwa kufululiza au kwa kuachanisha?

Jibu: Ndio, fadhilah zipo. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayefunga Ramadhaan kisha akaifuatishia siku sita za Shawwaal basi ni kama ambaye amefunga mwaka mzima.”[1]

Mtu anatakiwa azingatie kwamba fadhilah hii haipatikani isipokuwa mpaka kwanza amalize kufunga Ramadhaan yote. Kwa ajili hiyo mtu akiwa na deni la Ramadhaan basi anatakiwa kulifunga kwanza kisha ndio afunge siku sita za Shawwaal. Vinginevyo mtu hapati thawabu hizi, ni mamoja swawm imesihi au haikusihi. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayefunga Ramadhaan kisha akaifuatishia… “

Yule mwenye deni la Ramadhaan kunasemwa kuwa amefunga baadhi ya Ramadhaan na haisemwi kuwa amefunga Ramadhaan.

Siku hizi sita inafaa zikawa zenye kufuatana au zenye kuachana. Lakini hata hivyo kuzifululiza ndio bora zaidi, kwanza ni kuharakisha kufanya matendo ya kheri, jengine mtu anaepuka mambo ya kuchelewa ambayo yanaweza kupelekea mtu asikamilishe funga.

[1] Muslim (1164).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (20/17-18)
  • Imechapishwa: 06/06/2019