Ama kuhusu Hadiyth isemayo “Mimi ndio mji wa elimu na ´Aliy ndiye mlango wake”, ni dhaifu zaidi. Ndio maana inatajwa katika vile vitabu vinavyotaja Hadiyth zilizozuliwa ijapokuwa at-Tirmidhiy[1] ameipokea. Ibn-ul-Jawziy ameitaja[2] na amebainisha kwamba njia zake zote zimezuliwa. Uongo uko wazi kwenye Hadiyth yenyewe. Kwani ikiwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio alikuwa mji wa elimu na hakuna na mlango isipokuwa mlango mmoja tu na hakuna aliyefikisha kutoka kwake isipokuwa mtu mmoja tu, basi hiyo ina maana kwamba Uislamu ungeangamia.

Kwa ajili hiyo wanachuoni wote wameafikiana kwamba haijuzu mtu anayefikisha kutoka kwake akawa ni mmoja tu. Bali ni wajibu wale wafikishaji wakawa wengi tele wenye kuwafikishia wale wasiokuwepo. Upokezi wa mtu mmoja tu haufidishi elimu isipokuwa mpaka usapotiwe na viashirio (Qaraa-in) ambao unaweza kuwa haujafika au umefichikana kwa watu wengi. Kwa hivyo wanakosa elimu ya Qur-aan na Hadiyth zilizopokelewa kwa mapokezi mengi.

Wakisema kwamba mtu huyo mmoja amekingwa na kukosea na elimu inaweza kupatikana kwa maelezo yake, basi tutawaambia kwamba ni lazima wathibitishe kielimu juu ya kukingwa kwake na kukosea. Kukingwa kwake na kukosea hakuwezi kuthibitishwa kupitia maneno yake mwenyewe midhali mtu hatambui kuwa amekingwa na kukosea. Jambo hilo linaweza kuthibitishwa tu kwa maafikino, na maafikino hayapo katika suala hili. Kwa njia hiyo jambo lote linarudi juu ya kuthibitisha kukingwa kwake na kukosea kupitia madai yake mwenyewe. Hivyo inapata kufahamika kwamba lau kweli kukingwa kwake na kukosea ingelikuwa ni jambo la kweli, basi ni lazima hilo litambulike kwa njia zengine isiyokuwa maneno yake mwenyewe.

Kama kweli mji usingelikuwa na mlango isipokuwa kupitia kwake tu, basi kukingwa kwake na kukosea wala kitu kingine kinachohusina na dini kisingeliweza kuthibitishwa. Hivyo ikapata kutambulika kwamba Hadiyth hii imetungwa na mtu mjinga zindiki ambaye amedhania kuwa Hadiyth hii kuna kumsifu ndani yake. Bali uhakika wa mambo ni kwamba hiyo ni njia moja wapo ya kuutukana Uislamu kwani haukufikishwa isipokuwa na mtu mmoja peke yake.

[1] al-Albaaniy amesema: ”Imezuliwa.” (adh-Dhwa´iyfah (2955))

[2] Ibn-ul-Jawziy amesema: ”Hadiyth hii haina msingi.” (al-Mawdhuu´aat (1/261) na adh-Dhahabiy ameafikiana na hilo katika ”Talkhisw-ul-Mawdhuu´aat”, uk. 116)

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islam Ahmad bin Taymiyyah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Minhaaj-us-Sunnah an-Nabawiyyah (7/515)
  • Imechapishwa: 08/12/2018