Miongoni mwa dalili zilizotumiwa kwamba usiku wa Qadr sani usiku wa tarehe ishirini na saba ni zile dalili na alama na zile du´aa zinazoitikiwa zilizopokelewa juu ya usiku huo tangu hapo kale mpaka hii leo. Ubayy bin Ka´b amesema alama yake ni jua kuchomoza siku hiyo likiwa halina miale ya kuchoma. ´Abdah bin Abiy Lubaabah alikuwa akisema:

“Usiku wa Qadr ni usiku wa tarehe ishirini na saba.”

Amejengea hilo hoja kwa vitu mbalimbali, kukiwemo nyota. Imepokelewa na ´Abdur-Razzaq. Pia imepokelewa kutoka kwa ´Abdah kwamba alionja maji ya bahari usiku wa tarehe ishirini na saba na akayakuta ni matamu. Haya yametajwa na Imaam Ahmad kwa cheni ya wapokezi wake.

Baadhi ya Salaf walifanya Twawaaf katika Ka´bah usiku wa tarehe ishirini na saba na wakawaona namna ambavo Malaika walivokuwa wakizunguka hewani juu ya vichwa vya watu.

Abu Muusa al-Madiyniy amepokea kutoka kwa Abush-Shaykh al-Asbahaaniy kwa cheni ya wapokezi kutoka kwa Hammaad bin Shu´ayb ambaye amesema:

“Ilipofika zile siku kumi za mwisho nilikuwa ni mwenye kutazama usiku. Bwana mmoja akaniuliza ni nini ninachotafuta. Nikasema: “Usiku wa Qadr.” Ndipo akasema: “Lala. Hakika mimi nitakupasha khabari.” Ilipofika usiku wa tarehe ishirini na saba, akaja na kunishika mkono na akanipeleka kwenye mti wa mtende. Ulikuweko mti mmoja ambao jani lake limedondoka ardhini. Akasema: “Haya kwa mwaka hatuyaoni wakati wowote isipokuwa katika usiku huu.”

Abu Muusa amepokea kwa cheni za wapokezi wake jinsi bwana mmoja aliyepoza mwili mzima alivyomuomba Allaah du´aa kwenye usiku wa tarehe ishirini na saba. Baada ya hapo akaweza kutembea. Vivyo hivyo hayo yalimpitikia mwanamke mwingine aliyekuwa amepoza mwili mzima. Bwana mwingine Baswrah ambaye alikuwa bubu kwa miaka thelathini. Akamuomba Allaah du´aa usiku wa tarehe ishirini na saba. Baada ya hapo akaanza kuongea. Ibn Hubayrah amesimulia usiku wa kuamkia ijumaa wa tarehe ishirini na saba jinsi alivyoona mlango ulivofunguliwa mbinguni kaskazini mwa Ka´bah. Amesema:

“Nadhani kuwa ulikuwa juu ya chumba kitukufu cha Mtume.”

Hali iliendelea kuwa hivo mpaka alipogeuka upande wa mashariki ili atazame kama alfajiri imekwishachomoza. Pindi alipogeuka tena, akaona umekwishapotea. Amesema:

“Moja katika nyusiku hizi za witiri zikiangukia siku ya ijumaa, basi usiku huo ni wenye matarajio zaidi kuliko usiku mwingine wowote.”

Tambua kwamba alama zote hizi hazitoi dhamana juu ya usiku wa Qadr.

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Latwaa’if-ul-Ma´aarif, uk. 276-277
  • Imechapishwa: 14/05/2020