al-Albaaniy kuhusu kisa cha al-´Utbiy


al-Bayhaqiy amepokea katika “as-Shu´ab” (02/82/01/02) kwa cheni ya wapokezi wake kutoka kwa Abu Yaziyd ar-Ruqaashiy kutoka kwa Muhammad bin Ruuh bin Yaziyd al-Baswriy aliyesema: Ayyuub al-Hilaaliy amenihadithia:

“Kuna mbedui mmoja alihiji na wakati alipofika kwenye mlango wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akampigisha magoti mnyama wake na kumfunga kamba. Kisha akaingia msikitini mpaka akalifikia kaburi na akasimama usawa na uso wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akasema: “Namtoa fidia baba na mama yangu, ee Mtume wa Allaah! Nimekujia hali ya kuwa nimelemewa kwa madhambi na makosa. Nakuomba uombezi kwa Mola wako kwa sababu anasema katika Kitabu Chake:

وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذ ظَّلَمُوا أَنفُسَهُمْ جَاءُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّـهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّـهَ تَوَّابًا رَّحِيمًا

“Lau wao pale walipojidhulumu nafsi zao wangelikujia wakamuomba Allaah msamaha na Mtume akawaombea msamaha, basi wangelimkuta Allaah ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu.”[1]

Cheni ya wapokezi ni dhaifu na yenye giza. Simjui ni nani Ayyuub al-Hilaaliy wala walio chini yake. adh-Dhahabiy amemtaja Abu Yaziyd ar-Ruqaashiy katika ”al-Muqtanaa fiy Sard-il-Kunaa” pasi na kumtaja jina na akaashiria kuwa hatambuliki kwa maneno yake:

“Amenukuu kitu.”

Naona kuwa anaashiria cheni hii. Ni yenye munkari wa wazi. Inakutosha kutambua kwamba inarejea kwa mtu wa shambani asiyetambulika. Kwa masikitiko makubwa amekitaja Ibn Kathiyr katika tafsiri yake ya Aayah hii (04:64) na Ahl-ul-Ahwaa´ na wazushi wengi wamekichukua kutoka kwake. Mmoja wao ni as-Swabuuniy katika ufupisho wake wa “at-Tafsriyr” ya Ibn Kathiryr. Ndani yake kuna nyongeza mwishoni mwake:

“Kisha mbedui yule akaondoka na usingizi ukanishinda. Nikamuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) usingizini akasema: “Ee ´Utbiy, muwahi mbedui yule na umbashirie kwamba Allaah amemsamehe.”

Ibn Kathiyr hakukiegemeza kwa yeyote anayetambulika katika Ahl-ul-Hadiyth. Uhakika wa mambo ni kwamba amekiegemeza kwa al-´Utbiy pasi na cheni yoyote. Mtu huyo hatambuliki isipokuwa katika kisa hiki peke yake. Pengine yeye ndiye huyo Ayyuub al-Hilaaliy katika cheni ya al-Bayhaqiy.

Ni kisa ambacho ni munkari bali batili kwa sababu ya kwenda kwake kinyume na Qur-aan na Sunnah. Kwa ajili hiyo ndio maana kinaenezwa na Ahl-ul-Bid´ah kwa sababu kinajuzisha kumwomba ulinzi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumuomba uombezi baada ya kufariki kwake. Hii ni miongoni mwa batili kubwa kabisa, kama ambavo inafahamika. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amechukua jukumu la kubainisha jambo hilo katika vitabu vyake na khaswa “at-Tawassaul wal-Wasiylah”. Humo amekikaripia kisa hichi cha al-´Utbiy. Anaweza kurejea huko yule anayetaka utambuzi zaidi na elimu.

[1] 04:64

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swaahiyhah (6/2/1034)
  • Imechapishwa: 03/03/2021