97. Sampuli ya pili ya Ahl-ul-Hadiyth


Sampuli ya pili: Ahl-ur-Riwaayah wa Diraayah. Hawa ni wale wanachuoni ambao wamezielewa Hadiyth na wananyofoa hukumu kutoka katika Hadiyth hizo na vilevile kutaja uelewa wa Hadiyth. Mfano wa hawa ni kama al-Bukhaariy, Muslim, Maalik na Ahmad. Hawa ni wanachuoni wa Hadiyth. Wamezihifadhi na kuzielewa.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewapigia mfano watu hawa pale aliposema:

“Mfano wa yale niliyotumilizwa na Allaah katika uongofu na haki ni kama mfano wa mvua nyingi iliyonyesha katika ardhi ambapo ikawa nzuri, ikakubali maji na kuotesha nyasi na majani mengi. Sehemu nyingine ikawa ni kavu na ngumu inayozuia maji, Allaah akawanufaisha watu kwa mvua hiyo ambapo wakanywa [mifugo yao] na wakalima [kwa maji hayo]. Ikanyesha sehemu nyingine ambayo ni kame haizuii maji na wala haioteshi nyasi. Basi mifano hiyo ni mfano wa mtu aliyefahamu katika dini ya Allaah, Allaah akamnufaisha na yale aliyonituma kwayo, akajua na akafundisha [wengine]. Na mfano [wa aina hii ya mwisho] wa ambaye hakuliinulia hilo kichwa na wala hakuukubali uongofu wa Allaah niliotumwa nao.”[1]

Kundi la kwanza: … ni kama mfano wa mvua nyingi iliyonyesha… – Hawa ndio kama mfano wa  wenye kuhifadhi. Wamezidhibiti, wakazipokea na kuzihifadhi. Ambaye anahitajia dalili anaenda kwa wale walioziandika na wakazikusanya. Wanachota kutoka humo.

Kundi la pili: … Sehemu nyingine ikawa ni kavu na ngumu inayozuia maji… – Hawa ni kama mfano wa wasomi wa Hadiyth ambao wamezihifadhi Hadiyth, kuzidhibiti na wakanyofoa hukumu kutoka humo. Hawa wameotesha majani na watu wakanywa kutoka humo. Hawa ni bora zaidi kuliko kundi lililo kabla yake. Hawa ni bora zaidi kuliko wale waliohifadhi. Kwa sababu hawa ndio Ahl-ur-Riwaayah wa Diraayah.

Kundi la tatu: … Ikanyesha sehemu nyingine ambayo ni kame… – Huu ndio mfano wa yule ambaye hakukubali uongofu wa Allaah na hakuliinulia hilo kichwa. Watu wamegawanyika mafungu haya matatu:

1- Wamekubali. Hawaoteshi, lakini hata hivyo wamezuia maji. Hawa ndio wale wenye kuhifadhi.

2- Kundi lililozuia maji na kuotesha. Huu ndio mfano wa wale wenye kuhifadhi na wanachuoni.

3- Kundi lisilokuwa na kheri yoyote kabisa. Halioteshi majani na hawa halizuii maji. Huu ni kama mfano wa wanafiki ambao hakuna kheri yoyote ndani yao na wala hawainulii kichwa Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Watu bora katika Ummah ni Ahl-ul-Hadiyth. Wao ndio kundi lililookoka. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ikiwa kundi lililookoka sio Ahl-ul-Hadiyth basi sijui ni wepi.”[2]

Ahl-ul-Hadiyth ndio kundi lililookoka. Kadhalika anaingia katika wao yule ambaye atawafuata na akapita juu ya mfumo wao.

[1] al-Bukhaariy (79) na Muslim (15) na (2282)

[2] “Sharaf  Aswhaab-il-Hadiyth”, uk. 25 ya al-Khatwiyb al-Baghdaadiy