96. Sampuli ya kwanza ya Ahl-ul-Hadiyth


Mwandishi (Rahimahu Allaah) amesema:

39- Usiwe katika watu waliofanya dini yao ni pumbao

     ukawatukana na kawaponda Ahl-ul-Hadiyth

Ni juu yako kuwaheshimu Ahl-ul-Hadiyth. Ahl-ul-Hadiyth ndio watu wa mapokezi ambao wamezitilia umuhimu Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuzihifadhi mpaka wakawafikishia nazo watu kama zilivyokuja kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakazisafisha kutokana na kasoro zote. Wamezitilia umuhimu kikamilifu. Wamegawanyika sampuli mbili:

Sampuli ya kwanza: Ahl-ur-Riwaayah. Hawa ni wale wenye kuhifadhi mlolongo wa wapokezi wake, wakawa bingwa kwazo, wakapambanua baina ya wapokezi wake na wakabainisha hali za wapokezi. Kadhalika wakatilia umuhimu zile matini, wakazihifadhi na kuzifikisha kwa matamshi yake. Hali imekuwa namna hii kiasi cha kwamba mpaka pale ambapo yule mwenye kuhifadhi akitilia shaka juu ya tamko anasema:

“Au amesema hivi na vile.”

Anataja uwezekano wa pili na wala hakati moja kwa moja. Wakati mwingine husema:

“Fulani ametilia shaka.”

Anasema hivi hata kama tamko la pili litakuwa na maana ya lile tamko alilokomeka nalo. Haijalishi kitu hata kama maana itakuwa ni ile ile. Wanaheshimu matamko kwa njia ya kwamba wanaifikisha Hadiyth kwa tamko lake kama ilivyokuja kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Huku ni kutendea kazi maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah ampe nuru mtu ambaye atasikia maneno yetu akayafikisha kama alivyoyasikia. Huenda mfikishawaji anaelewa zaidi kuliko aliyesikia.”[1]

Wanahifadhi matini ya zile Hadiyth na mlolongo wa wapokezi wake ili kusiingie ndani yake matamshi yasiyokuwa ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Endapo watakuwa na shaka, basi wataibainisha. Vilevile wanazidurusu sanadi zake na kutambua hali za wapokezi mmoja baada ya mwengine. Hivyo wanabainisha kati ya ilio Swahiyh, nzuri, dhaifu na iliyotungwa. Hii ndio kazi kubwa ya wenye kuhifadhi. Wanaitwa “wakosoaji wa matini na mlolongo wa wapokezi.” Ni kama wakaguzi wa dhahabu na fedha. Ni kama sonara. Masonara wanajua dhahabu na fedha ya kweli na ya feki. Pale tu anaposikia sauti ya pesa anajua kuwa ni ya kweli au feki. Wasomi wa Hadiyth wanakuwa kama wao. Pindi tu wanaposikia Hadiyth na wakasikia mlolongo wa wapokezi wake wanakwambia hali yake. Hawa ndio wanachuoni wa mapokezi.

[1] Abu Daawuud (3660), at-Tirmidhiy (2656), Ibn Maajah (230), Ahmad (01/437) na wengineo