91. Dalili ya swalah na zakaah ndani ya Qur-aan


Dalili ya swalah ni pale aliposema (Ta´ala):

وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ

“Wasimamishe swalah.”

Maana yake ni kwamba mtu aiswali kama alivoiamrisha kwa sharti zake, nguzo zake na mambo yake ya wajibu. Kutekeleza amri kwa aina ya ile sura yake peke yake ni kitu hakitoshi. Ndio maana hakusema:

“Waswali.”

Bali amesema:

وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ

“Wasimamishe swalah.”

Swalah haiwi yenye kusimamishwa isipokuwa mpaka pale ambapo itaswaliwa kama alivyoamrisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kuhusu ambaye anaswali ile sura ya swalah kwa msemo mwingine wakati anaotaka, bila ya twahara, bila ya utulivu na wala asitekeleze vigezo vya swalah, mtu kama huyu hakuswali. Kwa ajili hii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia yule bwana aliyeswali vibaya na hakuwa na utulivu ndani ya swalah yake:

“Rejea ukaswali. Kwani hakika hukuswali.”[1]

Malengo sio ile sura ya swalah ambapo mtu akasimama, akarukuu, akasujudu na kuketi chini peke yake. Haya sio malengo. Bali malengo ni kuiswali kama alivyoamrisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hali ya kutimiza vigezo vyake vyote vya Kishari´ah.

Kisha akataja dalili ya zakaah pale aliposema (Ta´ala):

وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ

“… na watoe zakaah.”

Bi maana aitoe zakaah kuwapa wale wenye kuistahiki ambao Allaah amewataja katika maneno Yake:

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَابْنِ السَّبِيلِ ۖ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

“Hakika zakaah ni kwa ajili ya mafakiri na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao [kwa ajili ya Uislamu] na kuwakomboa mateka na wenye deni na katika njia ya Allaah na msafiri [aliyeharibikiwa] – ni faradhi itokayo kwa Allaah; na Allaah ni Mjuzi, Mwenye hekima.”[2]

Ametaja watu aina nane wenye kuistahiki kwa njia ya kufupiza. Mwenye kuwapa mbali na watu hawa nane basi anazingatiwa hakutoa zakaah ijapokuwa atatoa pesa nyingi mamilioni au mabilioni na akaziita kuwa ni zakaah. Haiwi zakaah mpaka iwekwe mahala pake ambapo amepafupiza Allaah. Jengine ni kwamba mtu anapaswa kuitoa ndani ya wakati wake ambapo imewajibika na asiicheleweshe.

[1] al-Bukhaariy (757) na Muslim (397).

[2] 09:60

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 188-190
  • Imechapishwa: 19/01/2021