88. Imani ya kuamini Mizani


Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Itawekwa mizani kwa ajili ya kupima matendo ya waja. Ambaye mizani yake itakuwa mizito, basi hao ndio wenye kufaulu.

MAELEZO

Miongoni mwa mambo ya lazima kuyaamini yatakayokuwa siku ya Qiyaamah ni Mizani ya matendo. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالْوَزْنُ يَوْمَئِذٍ الْحَقُّ ۚ فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُم بِمَا كَانُوا بِآيَاتِنَا يَظْلِمُونَ

“Kipimo kwa mizani siku hiyo itakuwa ni haki, basi ambao mizani yao itakuwa nzito, hao ndio watakaofaulu na ambao mizani yao itakuwa khafifu, basi hao ni wale waliokhasirika nafsi zao kwa yale waliyokuwa wakizifanyia dhuluma Aayah Zetu.”[1]

Katika Aayah nyingine imekuja:

وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ فِي جَهَنَّمَ خَالِدُونَ

“… na yule ambaye mizani [ya matendo] yake [mema] itakuwa khafifu, basi hao ni ambao wamekhasirika nafsi zao; Motoni ni wenye kudumu.”[2]

Mizani ina masahani mawili na ulimi. Matendo mema yatawekwa kwenye sahani moja na matendo maovu yatawekwa kwenye sahani nyingine. Sahani lenye matendo mema likuwa zito, basi mwenye nalo ataingia Peponi. Sahani lenye matendo maovu likiwa zito, basi mwenye nalo ataingia Motoni. Ni uadilifu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala); hamdhulumu yeyote.

Ni lazima kuamini mzani huu na kwamba ni mzani wa kweli na kwamba utapima matendo, kama alivyokhabarisha Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mu´tazilah wanasema kuwa ni mizani ya kimaana na sio mizani ya kikweli. Wao wanaona kuwa Mizani ni kinaya cha kutekeleza uadilifu siku ya Qiyaamah. Maneno haya ni batili na ni tafsiri mbovu. Haijuzu kuyapindisha maana maandiko sahihi na ya wazi ndani ya Qur-aan na Sunnah. Imani sio kukengeusha na kupindisha imani, kwa sababu imani inahusiana na kuyaamini yale yaliyokuja kutoka kwa Allaah na Mtume Wake Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya uhakika wake.

Mizani ni ya haki na juu yake yatapimwa matendo siku ya Qiyaamah. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَأَمَّا مَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَهُوَ فِي عِيشَةٍ رَّاضِيَةٍ وَأَمَّا مَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُمُّهُ هَاوِيَةٌ وَمَا أَدْرَاكَ مَا هِيَهْ نَارٌ حَامِيَةٌ

“Basi yule itakayekuwa mizani yake nzito, basi huyo atakuwa katika maisha ya kuridhisha. Na yule itakayekuwa mizani yake khafifu, basi makazi yake ni Haawiyah. Na nini kitakachokujulisha ni nini hiyo Haawiyah? Ni moto mkali mno wa mwako!”[3]

Inahusiana na Mizani; matendo mema na maovu ndio yatakayopimwa juu yake.

[1] 07:8-9

[2] 23:103

[3] 101:6-11

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 66-67
  • Imechapishwa: 23/08/2021