88. Dalili ya kushuhudia shahaadah ya pili


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, ni Kauli Yake (Ta´ala):

لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Hakika amekujieni Mtume anayetokana na nyinyi wenyewe, ni magumu juu yake yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni, mwenye huruma mno na mapenzi tele kwa waumini.”[1]

MAELEZO

Nguzo ya kwanza katika nguzo za Uislamu imejengeka juu ya mambo mawili:

La kwanza: Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah.

La pili: Kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah.

Mawili hayo ni nguzo moja. Sehemu ya kwanza inahusiana na kumtakasia ´ibaadah Allaah. Sehemu ya pili inahusiana na kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Dalili ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah ni maneno Yake (Ta´ala):

لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Hakika amekujieni Mtume anayetokana na nyinyi wenyewe, ni magumu juu yake yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni, mwenye huruma mno na mapenzi tele kwa waumini.”

Dalili zinazofahamisha kuwa Muhammad ni Mtume wa Allaah ni nyingi kutoka katika Qur-aan na Sunnah na miujiza mitukufu iliyofahamisha juu ya ujumbe wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Moja katika dalili kutoka katika Qur-aan ni Aayah hii:

لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Hakika amekujieni Mtume anayetokana na nyinyi wenyewe, ni magumu juu yake yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni, mwenye huruma mno na mapenzi tele kwa waumini.”

Huu ni ushuhuda kutoka kwa Allaah kwa Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya ujumbe na kubainisha sifa yake.

Amekujieni – Hapa wanazungumzishwa watu wote. Kwa sababu ujumbe wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni wenye kuenea kwa majini na watu; watu na majini.

Mtume – Ni yule ametumilizwa kwa Shari´ah na akaamrishwa kuifikisha. Kwa sababu ametumwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Anayetokana na nyinyi – Bi maana kutokana na  nyinyi watu. Sio Malaika miongoni mwa Malaika. Huu ni mwenendo wa Allaah (Subhaanah) huwatumilizia watu mjumbe anayetokana na wao kwa ajili ya ubainifu na ili aweze kuzungumza pamoja nao. Jengine ni kwa sababu wanamtambua. Endapo angewatumilizia Malaika wasingeweza kuzungumza pamoja naye kwa sababu hatokamani nao. Jengine ni kwamba hawawezi kumtazama Malaika. Kwa sababu hatokamani na umbile lao. Miongoni mwa huruma Yake (Subhaanahu wa Ta´ala) akawamutilizia watu Mtume anayetokana na umbile lao. Bali anayetokana na waarabu na anayetokana na nyumba tukufu zaidi za waarabu kiukoo. Anatokana na Banuu Haashim ambao ndio ukoo mtukufu zaidi wa Quraysh. Quraysh ndio ukoo mtukufu zaidi kwa waarabu. Kwa hiyo mbora katika wabora ambaye wanamtambua; wanatambua utu wake, ukoo wake, kabila lake na nchi yake. Wangelimsadikisha vipi ingelikua hawamjui? Wangejua vipi anachozungumza angelikuwa ni mwenye kuzungumza lugha isiyokuwa yao?

عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ

“… ni magumu juu yake yanayokutaabisheni.”

Bi maana juu yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Yanayokutaabisheni – Bi maana yanayokutieni ugumu. Maana yake ni magumu na mazito. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yanamtia uzito yale yanayowatia uzito Ummah wake. Alikuwa si mwenye kuutakia mazito. Bali alikuwa ni mwenye kuutakia wepesi na urahisi. Ndio maana Shari´ah yake ikaja na mambo mepesi. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimetumilizwa na Haniyfiyyah nyepesi.”[2]

Amesema (Ta´ala):

وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ

“Hakukufanyieni ugumu wowote ule katika dini.”[3]

مَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيَجْعَلَ عَلَيْكُم مِّنْ حَرَجٍ

”Allaah hataki kukufanyieni ugumu wowote.”[4]

Shari´ah yake ni nyepesi inayoendana pamoja na uwezo wa watu na wala haiwabebeshi yale wasiyoyaweza. Kwa ajili hii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwapendea wepesi. Hakupewa achague kati ya mambo mawili isipokuwa alichagua ambalo ni lepesi zaidi muda wa kuwa sio dhambi. Wakati fulani alikuwa anapenda kufanya kitendo lakini anakiacha kwa sababu ya kuwaonea huruma Ummah wake. Anaacha kufanya kitendo ingawa anapenda kukifanya katika matendo mema kwa sababu ya kuwaonea huruma Ummah wake. Hizi ni miongoni mwa sifa zake kwamba yanamtaabisha yale yanayoutaabisha Ummah wake, yanamfurahisha yale yanayoufurahisha na anafurahi kwa kufurahi kwake. Ambaye hizi ndio sifa zake hapana shaka kwamba haji isipokuwa kwa yaliyo na kheri na rehema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

حَرِيصٌ عَلَيْكُم

“… anakuhangaikieni… “

Bi maana juu ya kuongoka kwenu na kukuondosheni kutoka katika giza na kukuingizeni ndani ya nuru. Kwa ajili hiyo ndio maana alikuwa akistahamili mazito wakati wa kuwalingania watu kwa kutarajia kuongoka kwao na kuwaondosha kutoka katika giza na kuwaingiza katika nuru. Allaah amesema kumwambia:

لَعَلَّكَ بَاخِعٌ نَّفْسَكَ أَلَّا يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ

“Huenda utaiangamiza nafsi yako kwa huzuniko kwamba hawawi wenye kuamini.”[5]

Huenda ukaiangamiza nafsi yako wasipoamini kwa ajili tu ya kuwahuzunikia. Kwa hivyo usiwahuzunikie. Haya ni miongoni mwa ukamilifu wa kuwatakia kwake kheri (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

 بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“… mwenye huruma mno na mapenzi tele kwa waumini.”

Amemsifu kuwa na huruma na si msusuwavu:

فَبِمَا رَحْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ لِنتَ لَهُمْ ۖ وَلَوْ كُنتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ

”Basi ni kwa rehema kutoka kwa Allaah umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mjeuri mwenye moyo mgumu wangelikukimbia.”[6]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa siku zote ni mwenye unyenyekevu na mlaini kwa waumini, akiwainamishia mbawa zake na akiwapokea kwa bashasha, upendo, hisia na kwa wema. Hizi ni miongoni mwa sifa zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Allaah ametaja sifa tano juu ya Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

1- Ni mwenye kutokana nanyi.

2- Ni magumu juu yake yanayokutaabisheni.

3- Anakuhangaikieni.

4- Ni mwenye mpole mno kwa waumini.

5- Mwenye huruma kwao.

Ni sifa tano miongoni mwa sifa za Mtume huyu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amefanya upole na huruma ni kwa waumini peke yake. Kwa sababu yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni mshupavu kwa washirikina na wakaidi. Anakasirika kwa kukasirika kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ جَاهِدِ الْكُفَّارَ وَالْمُنَافِقِينَ وَاغْلُظْ عَلَيْهِمْ ۚ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ

“Ee Nabii! Fanya jihaad dhidi ya makafiri na wanafiki na kuwa mkali kwao. Na makazi yao ni Jahannam, na ubaya ulioje mahali pa kuishia.”[7]

Upole na huruma ni kwa waumini peke yao. Hivo ndivo wanavokuwa waumini wao kwa wao:

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ

“Muhammad ni Mtume wa Allaah. Na wale walio pamoja naye ni wakali zaidi dhidi ya makafiri wanahurumiana baina yao.”[8]

Hizi ndio sifa zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 09:128

[2] Ahmad (36/623) (22291).

[3] 22:78

[4] 05:06

[5] 42:03

[6] 03:159

[7] 09:73

[8] 48:29

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 174-180
  • Imechapishwa: 18/01/2021