73. Uwajibu wa kuitendea kazi Tawhiyd kwa moyo, vitendo na kwa ulimi

Tunakhitimisha maneno, Allaah (Ta´ala) akitaka, kwa masuala makubwa ambayo ni muhimu sana yanayofahamika kupitia yale tuliyotangulia tuliyotaja, lakini tutayagawa kutokana na ukubwa wake na kutokana na makosa yanayofanywa ndani yake.

Tunasema: “Hakuna tofauti ya kwamba Tawhiyd lazima iwe kwa moyo, ulimi na ´amali. Mtu akiacha kitu katika haya, hawi Muislamu. Akiijua Tawhiyd na asiifanyie kazi, ni kafiri mwenye inadi, kama kufuru ya Fir´awn na Iblisi na mfano wao. Hili hukosea watu wengi. Wanasema: “Kwa hakika hii ni haki. Tunafahamu hili na tunashuhudia ya kwamba ni haki, lakini hatuwezi kulifanya na watu wa mji wetu hayajuzu isipokuwa yale yenye kuafikiana na wao tu”, au mfano wa nyudhuru kama hizo. Na wala masikini huyu hajui kuwa wengi wa viongozi wa kufuru wanaijua haki na wanaiacha kwa kitu katika nyudhuru. Kama alivyosema (Ta´ala):

اشْتَرَوْا بِآيَاتِ اللَّـهِ ثَمَنًا قَلِيلًا

”Wamenunua Aayah za Allaah kwa thamani ndogo.” (at-Tawbah 09 : 09)

Na mfano wa Aayah kama hizo. Kama Kauli Yake:

يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ

”Wanamtambua kama wanavyowatambua watoto wao.” (al-Baqarah 02 : 146)

Akiifanyia kazi Tawhiyd kwa matendo ya dhahiri bila ya kuifahamu na wala haiamini ndani ya moyo wake, ni mnafiki na ni mtu wa shari kuliko kafiri wa kweli.

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ

“Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka la chini kabisa Motoni.” (an-Nisaa´ 04 : 145)

Na haya ni masuala ambayo ni makubwa na marefu yanakubainikia ukiyafikiria kwenye maneno ya watu. Utaona mtu mwenye kujua haki na anaacha kuifanyia kazi, kwa kukhofia maisha ya dunia au nafasi au anataka kumpaka mtu mafuta. Hali kadhalika utaona wenye kuifanyia kazi kwa nje na si kwa undani. Ukiwauliza nini wanachoitakidi ndani ya moyo, hawajui.

MAELEZO

Shaykh (Rahimahu Allaah) amemaliza kitabu hichi kwa masuala makubwa na muhimu ambayo ni wajibu kuyafahamu na kuyaelewa vizuri. Mtu akiyafahamu ndio ataona makosa ya watu katika ´Aqiydah. Masuala yenyewe ni kwamba:

Tawhiyd inakuwa kwa maneno, vitendo na kuamini. Ni lazima yapatikane mambo haya matatu. Yatapokusanyika mambo haya matatu ndio mtu anakuwa mpwekeshaji na mwenye kumuamini Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kukikosekana moja katika hayo mtu hawi muumini wala mpwekeshaji.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 117-118
  • Imechapishwa: 14/04/2017