73. Swalah ya kupatwa kwa jua wakati uliokatazwa

Swali 73: Wakati mwingine jua linapatwa baada ya alasiri. Je, swalah ya kupatwa kwa jua iswaliwe wakati wa makatazo? Vivyo hivyo swalah ya mamkuzi ya msikiti?

Jibu: Wanazuoni wamekinzana juu ya masuala hayo mawili. Maoni ya sawa ni kufaa kufanya hivo bali ni jambo limewekwa katika Shari´ah. Kwa sababu swalah ya kupatwa kwa jua na swalah ya mamkuzi ya msikiti ni miongoni mwa zile swalah zinazoswaliwa kutokana na sababu. Maoni ya sawa ni kwamba zimesuniwa wakati wa makatazo baada ya ´Aswr na baada ya Subh kama ilivyo wakati mwingine. Hilo ni kutokana na kuenea kwa maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika jua na mwezi ni alama mbili miongoni mwa alama za Allaah. Havipatwi kwa kufariki au kupata uhai kwa yeyote. Allaah kwavyo anawatia khofu waja Wake. Mkiona kitu katika hayo basi kimbilieni kumtaja, kumuomba, kumtaka msamaha, kutoa swadaqah, kuwaachia watumwa huru na kuswali misikitini mpaka iondoke hali hiyo.”

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Vilevile amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

 “Akiingia mmoja wenu msikitini basi asiketi chini mpaka kwanza aswali Rak´ah mbili.”

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Vivyo hivyo kuhusu Rak´ah mbili za Twawaaf pale ambapo muislamu akitufu baada ya Subh au ´Aswr. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Enyi wana wa ´Abdul-Manaaf! Msimzuie yeyote ambaye ametuku katika Nyumba hii na akaswali katika saa yoyote anayotaka ni mamoja usiku au mchana.”

Ameipokea Imaam Ahmad na watunzi wa Sunan wanne kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kupitia kwa Jubayr bin Mutw´im (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 77
  • Imechapishwa: 20/09/2022