11. ´Aqiydah sahihi juu ya muislamu mtenda dhambi

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaonelea kuwa hakuna dhambi, mbali na shirki, inayomtoa muislamu nje ya Uislamu isipokuwa pale atapoihalalisha. Ni mamoja akawa ni mwenye kuifanya na huku anaona kuwa ni halali au akawa anaamini kuwa ni halali pasi na kuifanya. Kwa sababu hii ina maana ya kwamba atakuwa ni mwenye kuikadhibisha Qur-aan na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), jambo ambalo ni kufuru kwa mujibu wa Kitabu, Sunnah na maafikiano.

Hakuna dhambi inayomfanya mwenye nayo kudumu Motoni milele isipokuwa tu shirki. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa, lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.” (04:48)

Aayah imefahamisha kuwa mtenda dhambi yuko chini ya matakwa ya Allaah; akitaka (Ta´ala) kumsamehe atamsamehe kwa fadhilah na ukarimu Wake, na akitaka atamwingiza Motoni kwa kiasi cha dhambi yake ili umsafishe na madhambi halafu baada ya hapo atamtoa kutokana na Tawhiyd yake kisha amwingize Peponi.

Allaah ametaja baadhi ya madhambi makubwa katika Kitabu Chake. Baadhi yake ni kuua na mashambulizi. Hata hivyo amethibitisha imani kwa wenye kufanya hivo. Mtu kama huyo ni muumini kwa imani yake, mtenda dhambi kwa dhambi zake. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِصَاصُ فِي الْقَتْلَى ۖ الْحُرُّ بِالْحُرِّ وَالْعَبْدُ بِالْعَبْدِ وَالْأُنثَىٰ بِالْأُنثَىٰ ۚ فَمَنْ عُفِيَ لَهُ مِنْ أَخِيهِ شَيْءٌ فَاتِّبَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ وَأَدَاءٌ إِلَيْهِ بِإِحْسَانٍ

“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Shari´ah ya kisasi waliouawa: muungwana kwa muungwana na mtumwa kwa mtumwa na mwanamke kwa mwanamke, na anayesamehewa na nduguye kwa lolote basi kufuatilizwa kwake kuwe kwa wema na kumlipa kwake iwe kwa wema.” (02:178)

Amemthibitishia (Ta´ala) imani yule muuaji na muuliwaji kama ambavyo amethibitisha kuwa ni wandugu katika imani. Hakuna mgongano wa kutumia neno “dhambi” katika kitendo au yule mtendaji, kumwita yule mtendaji muislamu na kumpitishia zile hukumu za Kiislamu juu yake. Kitu kinachoweka hilo wazi zaidi, ni kile kisa cha ´Abdullaah bin Himaar ambaye alikuwa anakunywa pombe. Pindi alipoletwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Swahabah mmoja akasema:

“Allaah akulaani. Ni wingi uliyoje unaletwa!” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Usimlaani; hakika anampenda Allaah na Mtume Wake.”

Dhambi hii haikumtoa nje ya Uislamu. Bali uhakika wa mambo ni kuwa alimthibitishia imani, pamoja na kutumbukia katika dhambi hii kubwa. Kitu kinachobainisha hilo, ni kuwa kufuru, shirki, dhuluma, dhambi na unafiki vimegawanyika aina mbili katika Shari´ah:

Aina kubwa: Aina hii ni ile inayomtoa mtu nje ya Uislamu.

Aina ndogo: Aina hii inapingana na ukamilifu wa imani wa yule mwenye nayo pasi na kumtoa nje ya Uislamu.

Mgawanyiko huu umebainishwa na Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum). Mmoja katika wabingwa wa Ummah na mfasiri wa Qur-aan, Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa), amesema kuwa kuna kufuru ndogo, dhuluma ndogo, dhambi ndogo na unafiki mdogo. Allaah amemwita yule mwenye kuomba badala Yake kwamba ni “kafiri”, “mshirikina” na “dhalimu”. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Na yeyote yule anayeomba pamoja na Allaah mungu mwengine hana ushahidi wa wazi wa hilo, basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake – hakika hawafaulu makafiri.” (23:117)

قُلْ إِنَّمَا أَدْعُو رَبِّي وَلَا أُشْرِكُ بِهِ أَحَدًا

“Sema: “Hakika mimi namuomba Mola wangu pekee na wala simshirikishi na yeyote.”” (72:20)

وَلَا تَدْعُ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُكَ وَلَا يَضُرُّكَ ۖ فَإِن فَعَلْتَ فَإِنَّكَ إِذًا مِّنَ الظَّالِمِينَ

“Wala usiombe badala ya Allaah asiyekufaa na wala asiyekudhuru. Endapo utafanya hivo, basi hakika utakuwa miongoni mwa madhalimu.” (10:106)

إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ فَفَسَقَ عَنْ أَمْرِ رَبِّهِ

“Isipokuwa Ibliys alikuwa miongoni mwa majini akaasi amri ya Mola Wake.” (18:50)

Haya yote yanahusiana na kufuru kubwa, shirki kubwa, dhuluma kubwa na dhambi kubwa ambavyo haviwezi kukusanyika na imani. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ

“Na yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio makafiri.” (05:44)

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ

“Na yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio madhalimu.” (05:45)

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ

“Na yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio mafasiki.” (05:47)

إِنَّ الَّذِينَ يَأْكُلُونَ أَمْوَالَ الْيَتَامَىٰ ظُلْمًا إِنَّمَا يَأْكُلُونَ فِي بُطُونِهِمْ نَارًا ۖ وَسَيَصْلَوْنَ سَعِيرًا

“Hakika wale wanaokula mali ya mayatima kwa dhuluma hapana shaka kwamba wanakula katika matumbo yao moto na watauingia Moto uliowashwa vikali.” (04:10)

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kumtukana muislamu ni dhambi na kumpiga vita ni kufuru.”

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kuapa kwa mwengine asiyekuwa Allaah amekufuru au ameshirikisha.”

Haya yanahusiana na kufuru ndogo, shirki ndogo, dhuluma ndogo na dhambi ndogo ambavyo vinaweza kukusanyika na imani, kama ilivyokuja katika Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya Salaf. Mambo haya yanafanya imani kupungua na kupingana na ukamilifu wake.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mu´taqad as-Swahiyh, uk. 71-75
  • Imechapishwa: 21/06/2020