68. Siku ya Mwisho


Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Hapana shaka yoyote Qiyaamah kitajitokeza.

MAELEZO

Miongoni mwa misingi ya imani ni pamoja na kuamini siku ya Mwisho. Ambaye ataikanusha basi ni kafiri. Washirikina wamepinga siku ya Mwisho, jambo ambalo ni ziada ya ukafiri wao. Hata wale ambao wanajidai kuwa ni waislamu lakini wanapinga jambo la kufufuliwa ni makafiri, kwa sababu wanamkadhibisha Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maafikiano ya waislamu na anapinga msingi miongoni mwa misingi ya imani.

Siku ya Mwisho ni ile siku ambayo dunia itamalizika. Dunia ndio siku ya kwanza na Qiyaamah ndio siku ya Mwisho. Ni lazima kuamini siku hiyo. Vilevile ni lazima kujiandaa juu ya siku hiyo. Kuiamini peke yake haitoshi. Mtu anatakiwa kujiandaa kwa ajili yake kwa kutenda matendo mema na kutubu juu ya madhambi yake ili aweze kufuzu siku hiyo.

Siku ya Mwisho huitwa pia kuwa ni Saa. Imekuja katika Qur-aan:

يَسْأَلُكَ النَّاسُ عَنِ السَّاعَةِ ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ اللَّـهِ ۚ وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّ السَّاعَةَ تَكُونُ قَرِيبًا

“Watu wanakuuliza kuhusu Saa. Sema: Ujuzi wake uko kwa Allaah. Na kipi kitakujulisha huenda Saa itakuwa karibu.”[1]

 Makusudio ya Saa ni ile siku ambayo dunia itakwisha na yanaanza maisha ya Aakhirah:

وَمَا أَمْرُ السَّاعَةِ إِلَّا كَلَمْحِ الْبَصَرِ أَوْ هُوَ أَقْرَبُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

”Na wala haikuwa amri ya Saa isipokuwa kama kupepesa kwa jicho au karibu zaidi. Hakika Allaah juu ya kila jambo ni Muweza.”[2]

Hukiambia kitu “Kuwa!” na kikawa. Saa na kipindi hicho hakuna anayekijua isipokuwa Allaah pekee. Lakini hata hivyo imesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba Saa itaangukia siku ya ijumaa[3].

[1] 33:63

[2] 16:77

[3] Muslim (854).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 52-53
  • Imechapishwa: 10/08/2021