61. Sura ya nne: Kuyatukuza masanamu vinyago na kuyatundika kwa ajili ya kumbukumbu

Masanamu vinyago ni wingi wa sanamu kinyago. Ni picha ya mwili kwa shakili ya mtu, mnyama au vyenginevyo katika vitu vyenye roho. an-Nuswb kimsingi ni sehemu au mawe ambapo washirikina walikuwa wakichinja sehemu hiyo. Masanamu ya ukumbusho ni yale masanamu yanayowekwa katika viwanja na sehemu mfano wake kwa ajili ya kuhuisha kumbukumbu ya kiongozi au mkuu.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametahadharisha kuvichukua picha viumbe vyenye roho na khaswa kuwachukua picha watu wanaoadhimishwa kama vile wanachuoni, wafalme, wachaji, viongozi na maraisi.  Ni mamoja picha hiyo ni kwa njia ya uchoraji kwenye ubao, kwenye karatasi, ukutani, kwenye nguo, kwa njia ya kuchukua picha kwa vifaa vya kisasa vya zama hizi au kwa njia ya kuchonga na kuitengeneza picha kwa sifa ya sanamu. Amekataza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutundika picha kwenye ukuta na mfano wake. Kunaingia vilevile yale masanamu ya ukumbusho. Kwa sababu hiyo ni njia inayopelekea katika shirki. Hakika shirki ya kwanza kujitokeza ulimwenguni ilikuwa ni kwa sababu ya picha na kutengeneza masanamu vinyago. Katika wakati wa Nuuh kulikuweko watu wema. Walipofariki watu wake wakahuzunika ambapo shaytwaan akawashawishi kutengeneza katika vikao vyao walivyokuwa wakikaa masanamu vinyago na wawaite kwa majina yao, jambo ambalo walilifanya lakini hayakuabudiwa. Mpaka walipofari watu wa kipindi kile na elimu ikasahaulika ndipo yakaabudiwa[1]. Pindi Allaah alipomtuma Mtume Wake Nuuh (´alayhis-Salaam) kukataza shirki hii iliyojitokeza kwa sababu ya picha hizo walizotengeneza watu wake wakakataa kukubali ulinganizi wake na wakaendelea kuziabudu picha hizo walizozitengeneza ambazo baadaye ziligeuka kuwa masanamu:

وَقَالُوا لَا تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلَا تَذَرُنَّ وَدًّا وَلَا سُوَاعًا وَلَا يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْرًا

“Wakasema: “Msiwaache waungu wenu na wala msimwache Wadd na wala Suwaa´ na wala Yaghuuth na Ya’uuq na Nasr!”[2]

Haya ni majina ya waja wale wema ambao walitengenezewa picha hizo kwa shakili zao kwa lengo la kuhuisha ukumbusho wao na kuwaadhimisha. Tazama lilivyokuwa mwisho wa jambo kwa sababu ya masanamu hayo ukumbusho katika kumshirikisha Allaah na kuwakaidi Mitume Yake, jambo ambalo lilisababisha kuangamizwa kwa mafuriko, kuchukiwa na Allaah na viumbe Wake. Mambo hayo yanakuonyesha ukhatari wa picha na kutengeneza sanamu kinyago. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawalaani watengeneza mapicha, akaeleza kwamba ndio watu wenye adhabu kali siku ya Qiyaamah, akaamrisha kuzipasuapasua picha na akakhabarisha kuwa Malaika hawaingii kwenye nyumba ilio na picha ndani yake. Yote hayo ni kwa sababu ya maharibifu yake na ukhatari wake mkubwa juu ya Ummah katika ´Aqiydah zao. Kwani shirki ya kwanza kujitokeza ulimwenguni ni kwa sababu ya kutengenezwa picha hizi vinyago. Haijalishi kitu utengenezwaji wa picha hizi na masanamu yanakuwa katika vikao, viwanja au mabustani. Kishari´ah ni mambo ya haramu. Kwa sababu ni njia inayopelekea katika shirki na yanaiharibu ´Aqiydah. Ikiwa makafiri hii leo wanayafanya mambo hayo – kwa sababu wao hawana ´Aqiydah wanayoichunga – basi haijuzu kwa waislamu kujifananisha nao na kushirikiana nao katika kitendo hichi kwa ajili ya kuhifadhi ´Aqiydah yao ambayo ndio chanzo cha nguvu na mafanikio yao. Haitakikani kusemwa kwamba watu wamepita hatua hii na wameitambua ´Aqiydah na shirki. Kwani shaytwaan hutegezea kizazi kinachokuja huko mbele wakati ujinga utapoenea kati yao, kama alivofanya kwa watu wa Nuuh pindi walipofariki wasomi wao na ujinga ukaenea kati yao. Isitoshe fitina haiaminiwi kwa ambaye bado yuko hai, kama alivosema Ibraahiym (´alayhis-Salaam):

وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الْأَصْنَامَ

“Uniepushe mimi na wanangu kuabudu masanamu.”[3]

Akachelea fitina juu ya nafsi yake. Baadhi ya Salaf wamesema:

“Ni nani mwenye kujiaminisha na mitihani baada ya Ibraahiym?”[4]

[1] al-Khattwaabiy ndio ametaja Athar hii katika ”al-Ghunyah ´an al-Kalaam wa Ahlihi”, uk. 22. Lakini asili ya Hadiyth iko katika Swahiyh-ul-Bukhaariy (4636).

[2] 71:23

[3] 14:35

[4] ad-Daar al-Manthuur (05/46).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 115-116
  • Imechapishwa: 24/03/2020