57- Kumswalia maiti wa Kiislamu ni faradhi kwa baadhi ya watu. Ameamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) jambo hilo. Nitataja katika Hadiyth hizo Hadiyth ya Zayd bin Khaalid al-Juhaniy:

“Kuna bwana mmoja katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikufa siku ya Khaybar. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatajiwa jambo hilo ambapo akasema: “Mswalieni rafiki yenu.” Nyuso za watu zikageuka kwa jambo hilo. Akasema: “Hakika rafiki yenu alichukua ngawira kabla hazijagawanywa.” Tukakagua vitu vyake alivokuwa navyo ambapo tukakuta mawe ya thamani katika mawe ya mayahudi hayana thamani ya dirhamu mbili.”

Ameipokea Maalik katika “al-Muwattwa´” (02/14), Abu Daawuud (01/425), an-Nasaa´iy (01/278), Ibn Maajah (02/197), Ahmad (04/114-05/192) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. al-Haakim amesema:

“Ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim.” Ndani yake kuna kasoro ambayo nimeibainisha katika “at-Ta´liyqaat al-Jiyaad ´alaa Zaad-il-Ma´aad”.

Kumepokelewa Hadiyth kutoka kwa Abu Qataadah kuhusiana na maudhui haya ambayo itakuja katika masuala yafuatayo, uk. 82, pia katika maudhui haya imekuja Hadiyth kutoka kwa Abu Hurayrah, uk. 84.

58- Wanavuliwa katika hayo watu wawili ambao sio lazima kuwaswalia:

1- Mtoto ambaye hajabaleghe. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumswalia Ibraahiym (´alayhis-Salaam). ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Ibraahiym, mvulana wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), alikufa akiwa na miezi kumi na nne, lakini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumswalia.”

Ameipokea Abu Daawuud (02/166) kupitia njia yake, Ibn Hazm (05/185), Ahmad (06/267) kwa cheni ya wapokezi nzuri. Kama alivosema al-Haafidhw katika “al-Iswaabah”. Pia Ibn Hazm amesema:

“Khabari hii ni Swahiyh.”[1]

2- Aliyekufa shahidi. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwaswalia mashahidi wa Uhud na wengineo. Kumepokelewa juu ya hayo Hadiyth tatu ambazo zimetangulia kutajwa katika masuala ya 32, ukurasa wa 25.

Lakini hayo hayapingani na usuniwaji wa kuwaswalia watu wawili hao pasi na ulazima. Zitakuja Hadiyht juu ya wawili hao katika masuala yanayofuata:

[1] Maoni ya sawa ni yale yaliyosemwa na al-Haafidhw. Ibn-ul-Qayyim katika ”Zaad-ul-Ma´aad” (01/203) ametaja kutoka kwa Imaam Ahmad kwamba amesema:

”Hadiyth hii ni munkari.”

Pengine anakusudia kwamba ni Hadiyth iliopokelewa kutoka kwa mtu mmoja. Kwani haya yamepokelewa kutoka kwake katika baadhi ya Hadiyth ambazo usahihi wake unatambulika vyema.

Tambua kwamba hakuna dosari inayoingia katika kuthibiti kwa Hadiyth hii kwamba imepokelewa kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alimswalia mvulana wake Ibraahiym. Kwa sababu hayo hayakusihi kutoka kwake ingawa yamepokelewa kutoka katika njia mbalimbali. Kwani njia zote hizo zina dosari ya Irsaal au udhaifu mkubwa kama utavyoona jambo hilo kwa upambanuzi katika “Naswb-ur-Raayah” (02/279-280).

Ahmad (03/281) amepokea kupitia kwa Anas kwamba aliulizwa: “Je, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimswalia mwanawe Ibraahiym?” Akajibu: “Sijui.” Cheni ya wapokezi Swahiyh.

Endapo angelikuwa amemswalia basi hilo lisingefichika kwa Anas – Allaah akitaka. Kwani alimtumikia miaka kumi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 103-104
  • Imechapishwa: 14/07/2020