Mshahara juu ya kazi ya uimamu, uadhini na ualimu

Swali: Mimi ni kijana ninayetamani kuwa imamu wa msikiti kwa sababu nina uwezo wa kufanya hivo. Lakini mimi nachelea juu ya nafsi yangu juu ya mshahara huu khofu dunia isije kuingia moyoni mwangu na hamu yangu kubwa ikawa kuwa mshahara tu.

Jibu: Usifanye hamu yako kubwa ni mshahara. Ifanye hamu yako uwe kiongozi wa wachaji Allaah. Wale wanaohudhuria misikitini ni miongoni mwa wanaomcha Allaah – Allaah akitaka. Wewe ndiye kiongozi wao. Kwa hivyo unaingia katika uenewaji wa maneno Yake (Ta´ala):

وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا

“Tujaalie kuwa waongozi kwa wenye kumcha Allaah.”[1]

Achana na mambo ya mshahara. Mshahara ukija ni sawa na usipokuja isiwe ndio hamu yako. Ukiwa hivo nia yako itakuwa safi.

Kule kuwatengea mishahara maimamu, waadhini na waalimu ni kwa ajili ya kutaka kuwashaji´isha juu ya kheri. Ni jambo la sawa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika vita vyake alikuwa akijaalia kitu kwa ajili ya kutaka kuwachangamsha wapiganaji juu ya mapigano. Mpaka alifikia kusema:

“Mwenye kuua muuaji basi ana mateka yake.”

Bi maana yale mavazi yake, kipando chake na mengineyo ambayo yanazingatiwa kuwa ni mateka. Yote haya ni kwa ajili ya kutaka kuwashaji´isha juu ya kheri. Hakuna vibaya kwa mtu kupokea bila yeye kuomba. Tatizo ni pale yeye atakapoomba azidishiwe juu ya kazi ya kidini. Kwa ajili hii Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) aliulizwa kuhusu mtu aliyeombwa awaswalishe watu Tarawiyh ambapo akawauliza atawaswalisha kwa kiwango cha pesa ngapi. Imamu Ahmad alipoulizwa kuhusu hili akasema:

“Ni nani awezaye kuthubutu kuswali nyuma ya mtu huyu?”

Maana yake ni kwamba mtu huyu anataka kuwa imamu kwa ajili ya dunia. Imaam Ahmad akamomba ulinzi kwa Allaah na akashangazwa na yule ambaye ataswali nyuma yake.

Kuna baadhi ya watu wanaonelea kuwa kile kitendo cha kupokea kwake mshahara juu ya uimamu kunapunguza kumtakasia kwake nia Allaah. Hili si sahihi. Ni kweli kunapunguza kumtakasia kwake nia Allaah ikiwa hawaswalishi isipokuwa kwa ajili ya mshahara huo. Ama ikiwa anawaswalisha kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall) na akajisaidia kwa kile atachokipokea juu ya mahitajio yake ya kidunia hakuna ubaya wa kufanya hivo.

[1] 25:74

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (38) http://binothaimeen.net/content/874
  • Imechapishwa: 14/07/2020