55. Radd kwa mwenye kudai kwamba kuwaomba du´aa na kinga watu wema sio ´Ibaadah II

mwambie: “Wewe unakubali kuwa Allaah kafaradhisha juu yako kumtakasia ´Ibaadah na ni haki Yake juu yako?” Akisema: “Ndio”. Mwambie: “Nibainishie hili ulilofaradhishiwa juu yako, ambalo ni kumtakasia ´Ibaadah Allaah pekee, jambo ambalo ni haki Yake juu yako!” Ikiwa hajui ´Ibaadah ni kitu gani na wala aina zake, basi mbainishie yale Allaah (Ta´ala) anayosema:

ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ

”Muombeni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa khofu. Hakika Yeye hawapendi wale wenye kuchupa mipaka.” (al-A´raaf 07 : 55)

Ukishamjulisha hayo, mwambie: “Unajua sasa kuwa hii ni ´Ibaadah?” Hana budi kusema: “Ndio” – na du´aa ndio kichwa cha ´Ibaadah. Mwambie: “Ikiwa umekubaliana na mimi ya kwamba ni ´Ibaadah na ukamuomba Allaah usiku na mchana, kwa khofu na unyenyekevu, kisha ukamuomba haja hiyo Mtume au mwengine; je utakuwa umeshirikisha katika ´Ibaada ya Allaah asiyekuwa Yeye?” Hana budi kusema: “Ndio”.

MAELEZO

Muulize nini maana ya ´ibaadah na ni ipi tofauti kati ya hayo mawili na kuomba kinga. Muulize kama ´ibaadah ni kitu cha wajibu au ni kitu tu kilichopendekezwa. Ni lazima akubali ya kwamba ´ibaadah ni jambo la wajibu na kwamba ni haki ya Allaah juu ya waja. Akiyakubali haya basi mwambie akufasirie nini maana ya ´ibaadah na akubainishie aina zake. Midhali umetambua kuwa ni kumuabudu Allaah na kwamba ni wajibu kwa mja, basi ni wajibu kwako kujua maana yake na utambue aina zake. Vinginevyo ni vipi Allaah atakuwajibishia kitu na wewe hukijui wala hukitambui? Mtu huyu hajui ´ibaadah ni nini na ni zipi aina zake. Huu ndio ugonjwa wa ujinga. Kuanzia hapa ni wajibu kwa kila mja kujifunza yale Allaah aliyomuwajibishia na kumfaradhishia ili aweze kuitekeleza kwa njia sahihi na kujiepusha na yale yenye kuitia kasoro au kuibatilisha kabisa. Ama kumuabudu Allaah kwa ujinga, huu ni mfumo wa manaswara wanaomuabudu Allaah kwa ujinga na upotevu. Allaah amekuamrisha umuombe akuepushe na mfumo wao pale unaposema:

اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ

“Tuongoze njia iliyonyooka; njia ya wale Uliowaneemesha, si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea.” (01:06-07)

Wapotevu ni wale wanaomuabudu Allaah pasi na elimu na pasi na kujua ´ibaadah. Wanamuabudu Allaah kwa desturi, kufuata kichwa mchunga na yale waliyowakutaemo mababa zao na mababu zao bila ya kurejea katika yale waliyokuja nayo Mitume na yakateremshwa na vitabu. Hii ndio sababu ya upotevu.

Kuomba kinga ni kule kuomba ulinzi kutokana na jambo lenye kutia khofu ambalo hakuna awezae kulizuia isipokuwa Allaah pekee. Ni aina moja wapo ya ´ibaadah. Allaah (Subhanaahu wa Ta´ala) ndiye alindae na wala hakilindwi chochote kinyume Naye na anamlinda yule mwenye kumuomba kinga. Kwa hivyo yule mwenye kumuomba kinga maiti amemuabudu badala ya Allaah. Vilevile miongoni mwa aina kubwa za ´ibaadah ni du´aa kwa kuwa Allaah (Ta´ala) amesema:

ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ

”Muombeni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa khofu. Hakika Yeye hawapendi wale wenye kuchupa mipaka.” (07:55)

Wewe umemuomba kinga asiyekuwa Allaah. Kwa hiyo umemuomba asiyekuwa Allaah, kitendo ambacho ni shirki.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 82-83
  • Imechapishwa: 10/01/2017