55. Mwenye kuomba kitu kwa jina la Allaah asirudishwe nyuma


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuomba kwa jina la Allaah mpeni, mwenye kujilinda kwa jina la Allaah mlindeni, mwenye kukuiteni muitikieni na anayekufanyieni wema mlipeni wema. Msipopata cha kumlipa muombeeni du´aa mpaka muone kweli kwamba mmemlipa wema.”[1]

Ameipokea Abu Daawuud na an-Nasaa´iy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

MAELEZO

Mwandishi ametaja mlango huu kwa sababu ndani yake kuna kumuadhimisha na kumtukuza Allaah kwa kule kumpa yule mwenye kuomba kwa jina la Allaah. Hadiyth ya Ibn ´Umar ni mfano wa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambayo ni machache lakini yaliyobeba maana kubwa.

1- Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuomba kwa jina la Allaah mpeni, mwenye kujilinda kwa jina la Allaah mlindeni, mwenye kukuiteni muitikieni na anayekufanyieni wema mlipeni wema. Msipopata cha kumlipa muombeeni du´aa mpaka muone kweli kwamba mmemlipa wema.”

Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kuomba kwa jina la Allaah mpeni… “

Haya ni kwa ajili ya kumuadhimisha na kumtukuza Allaah. Hata hivyo kumekuja Hadiyth nyingi zinazoonyesha kuwa imechukizwa kuomba kwa jina la Allah kwa sababu ni kuwatia watu katika uzito. Lakini hata hivyo ni wajibu kumpa yule mwenye kuomba haki yake kama mfano wa zakaah au akaomba kutoka katika mfuko wa mali ya waislamu. Mbali na hayo bora ni kumpa. Pamoja na hivyo haitakikani kwake kuomba kwa jina la Allaah kwa sababu ya kutendea kazi zile Hadiyth zinazoonyesha kuwa kitendo hicho kimechukizwa.

Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kujilinda kwa jina la Allaah mlindeni… “

Mwenye kuomba ulinzi kwa jina la Allaah basi ni jambo limewekwa katika Shari´ah kumlinda. Kwa ajili hii wakati ´Amrah bint al-Juun alipomwomba Allaah ulinzi dhidi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Hakika umeomba ulinzi kwa aliye Mtukufu. Rudi kwa familia yako.”[2]

Kama tulivosema ni jambo limewekwa katika Shari´ah kumlinda yule mwenye kuomba ulinzi kwa jina la Allaah midhali yuko katika haki. Ama akiomba ulinzi kwa jina la Allaah kwa ajili ya kukwepa haki yenye kumuwajibikia kama vile kuswali, kutoa zakaah, madeni au kafara mbalimbali, basi hatakiwi kulindwa na kusalimishwa.

Akiomba ulinzi kwa jina la Allaah kutohitajia kufanya kazi kama hakimu, kiongozi au kitu kingine miongoni mwa kazi ambazo ni khatari na wakati huohuo wakawepo wastahiki wengine wanaoweza kusimamia kazi hizo, basi imewekwa katika Shari´ah kumlinda na kumsalimisha. Kama ilivyopokelewa kwamba wakati ´Uthmaan alipomwamrisha Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhum) kufanya kazi kama hakimu aliomba kinga kwa jina la Allaah kusimamia jambo hilo ambapo ´Uthmaan akamlinda. Haya ikiwa yamesihi basi ni pale ambapo wapo wengine wastahiki ambao wanaweza kusimamia kazi hizo. Wakati wa ´Uthmaan walikuwepo wengi ambao wanaweza kusimamia kazi hizo.

Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… mwenye kukuiteni muitikieni.”

Kuitikia mwaliko ni jambo ambalo ndani yake kuna manufaa, kuunga udugu, urafiki na ukaribu. Kwa ajili hiyo ndio maana imewekwa katika Shari´ah kuitikia mwaliko ni mamoja ni mwaliko wa harusi au mwaliko mwingine. Hata hivyo mwaliko muhimu zaidi ni ule wa harusi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Asiyeitikia mwaliko basi amemuasi Allaah na Mtume Wake.”[3]

Ni wajibu kuitikia mwaliko isipokuwa kama kutakuwepo vipingamizi katika hali mbili:

1- Kukawepo kikwazo kama vile maradhi, ni mbali na kuna uzito kwake.

2- Kukawepo kikwazo kama mfano wa muziki, nyimbo na pombe.

Ama ikiwa mwaliko umesalimika basi ni wajibu au angalau tunaweza kusema kwamba imekokotezwa sana kuitikia. Hata hivyo haiwajibiki kuitikia mwaliko isipokuwa pale ambap mtu mwenyewe ataupokea.

Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Anayekufanyieni wema mlipeni wema. Msipopata cha kumlipa muombeeni du´aa mpaka muone kweli kwamba mmemlipa wema.”

Kumlipa mtu wema aliyokufanyia ni miongoni mwa tabia nzuri na ni miongoni mwa ukamilifu wa imani. Ikiwa mtu anaweza kulipa wema kwa pesa, afanye hivo. Kama haliwezi hilo basi afanye hivo kwa maneno mazuri na du´aa.

Haifai kuziomba sifa za Allaah kitu chochote kama mfano kuomba kwa uso Wake au ujuzi Wake. Hata hivyo inafaa kumuomba Allaah kwa majina na sifa Zake kama vile Mwingi wa huruma. Inafaa kufanya Tawassul kwa sifa za Allaah na sio kuziomba. Shaykh-ul-Islaam amenukuu maafikiano juu ya hilo. Mtu anaweza kuzitumia sifa Zake wakati wa kufanya maombi kwa mfano akasema:

“Nakuomba kwa msamaha Wako na huruma Yako na nakuomba ulinzi kwa radhi Zako kutokamana na hasira Zako.”

[1] Abu Daawuud (1672), an-Nasaa’iy (2567), Ahmad (5365), al-Bukhaariy katika ”al-Adab al-Mufrad” (216) na at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” (13465). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (1468).

[2] al-Bukhaariy (5254).

[3] al-Bukhaariy (5177) na Muslim (1432).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 156-157
  • Imechapishwa: 07/11/2018