52- Inafaa kupanda kipando kwa sharti watu watembelee nyuma yake. Hilo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mpandaji atatembea nyuma ya jeneza… “

Imekwishatangulia kwa utimilifu wake katika masuala ya 50.

Lakini bora ni kutembea kwa miguu. Kwa sababu hilo ndilo lililozoeleka kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wala haikupokelewa kwamba alipanda wakati wa kusindikiza. Bali Thawbaan (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliletewa kipando akiwa pamoja na jeneza lakini akakataa kumpanda. Wakati alipomaliza akaletewa kipando akampanda. Akaulizwa ambapo akajibu: “Hakika Malaika walikuwa wanatembea na sikuweza kupanda ilihali wao wanatembea. Walipoondoka ndipo nikapanda.”

Ameipokea Abu Daawuud (02/64-65), al-Haakim (01/355), al-Bayhaqiy (04/23). al-Haakim amesema:

“Ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim” na adh-Dhahabiy ameafikiana naye. Mambo ni kama walivosema.

Katika moja ya mapokezi ya al-Haakim na wengine kutoka kwa Thawbaan ambaye amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka katika jeneza akawaona watu wamepanda vipando ambapo akasema: “Je, hivi hamuoni haya! Hakika Malaika wa Allaah wanatembea kwa miguu yao ilihali nyinyi mko juu ya migongo ya wanyama.”

Cheni ya wapokezi wake ni dhaifu. Pia imepokelewa hali ya kuishilia kwa Swahabah. al-Bayhaqiy amesema:

“Hilo ndio sahihi zaidi.”

Mzunguko wa hilo limepokelewa hali ya kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hali ya kuishilia kutoka kwa Swahabah juu ya Abu Bakr bin Maryam ambaye ni dhaifu.

53- Inafaa kupanda kipando baada ya kumaliza mazishi pasi na kuwa machukizo yoyote. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Thawbaan iliyotajwa punde tu. Mfano wake ni Hadiyth ya Jaabir bin Samurah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimswalia Ibn-ud-Dahdaah [na sisi tulikuweko] [Katika upokezi mwingine imekuja: “Alitoka kusindikiza jeneza la Ibn-ud-Dahdaah [hali ya kutembea]. Kisha akaletewa farasi aliyetandikwa juu ambapo bwana mmoja akamfunga kisha akampanda [pindi walipomaliza] akawa anatembea na kuzikurubisha hatua zake na sisi tukiwa ni wenye kumfuata tunatembea nyuma yake. [Katika upokezi mwingine imekuja: “Pambizoni mwake.”] Bwana mmoja katika watu wale akasema: “Hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Ni matawi mangapi yaliyotundikwa au yaliyoinama Peponi ya Ibn-ud-Dahdaah!”

Ameipokea Muslim (03/60-61) na mtiririko ni wake, Abu Daawuud (02/65), an-Nasaa´iy (01/284), at-Tirmidhiy (02/138) ambaye ameisahihisha. Ameipokea pia al-Bayhaqiy (04/22-23), at-Twayaalisiy (760-761), Ahmad (05/98-99, 102) kupitia njia kutoka kwa Simaak bin Harb ambaye amepokea kutoka kwake.

Upokezi wa pili ni wa an-Nisaa´iy. Ziada ilioko ni ya at-Tirmidhiy kwenye moja katika mapokezi yake. Maana yake imekuja kwa at-Twayaalisiy.

Upokezi wa tatu ni wa Abu Daawuud na at-Tirmidhiy. Pia anayo Muslim, al-Bayhaqiy na Ahmad katika moja ya mapokezi yao.

Upokezi wa kwanza ni wa an-Nasaa´iy na mwingine ni wa Abu Daawuud.

Hili ni andiko la wazi kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipanda baada ya kumaliza mazishi, jambo ambalo limefichika kwa Abut-Twayyib Hasan Khaan ambapo akatumia hoja katika “ar-Rawdhwah” (01/173) kwamba yule anayesindikiza jeneza yuko na khiyari kati ya kutembea mbele yake au nyuma yake kutokana na Hadiyth hii akasema:

“Hakika Maswahabah walikuwa wakitembea pambizoni mwa jeneza la Ibn-ud-Dahdaah, jambo ambalo ni kosa kwa njia mbili:

1- Katika Hadiyth hakuna jambo alilotaja. Bali imesema wazi kwamba walikuwa wakitembea pambizoni mwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakuna kulazimiana kati ya mambo hayo mawili kama ilivyo dhahiri.

2- Hilo limetosha wakati wa kumaliza mazishi kama ilivyokwishatangulia. Huenda sababu ya kukosea huku ni upokezi wa ´Umar bin Muusa bin al-Wajiyh kutoka wa Simaak kwa Hadiyth hiyo kwa tamko lisemalo:

“Nilimuona Mtume wa Allaah (Sw alla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisindikiza jeneza la Thaabit bin ad-Dahdaah akiwa juu ya farasi mwenye baka jeupe kichwani mwake mwenye mabaka miguuni na mikononi mwake ambaye hakuwa na soga akiwa pamoja na watu nao wakiwa pambizoni mwake. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akashuka ambapo akamswalia kisha akakaa chini mpaka walipomaliza. Halafu akasimama na kukaa juu ya farasi wake akaondoka na watu wakiwa ni wenye kutembea pambizoni mwake.”

Ameipokea Ahmad (05/99). Hadiyth hii iko wazi juu ya kwamba inafaa kupanda kipando hata wakati wa kumsindikiza. Lakini kwa mtiririko huu ni batili. Kwa sababu ´Umar bin Muusa huyu alikuwa akitunga Hadiyth. Kwa hivyo hatumiwi kama hoja wakati wa kuafikiana kwa mapokezi sembuse wakati mapokezi ni yenye kutofautiana.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 96-99
  • Imechapishwa: 08/07/2020