Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ

“Miongoni mwa alama Zake ni kwamba amekuumbieni katika jinsi yenu wake ili mpate utulivu kwao na amekujaalieni kati yenu mapenzi na huruma. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaotafakari.”[1]

وَأَنكِحُوا الْأَيَامَىٰ مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُمْ ۚ إِن يَكُونُوا فُقَرَاءَ يُغْنِهِمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ ۗ وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ

“Waozesheni wajane miongoni mwenu na walio wema kati ya watumwa wenu wanaume na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Allaah basi Atawatajirisha katika fadhila Zake. Allaah ni Mwenye wasaa, Mjuzi wa yote.”[2]

Imaam Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) amesema:

“Haya ni kuwaozeshwa wanaume. Wapo wanachuoni wenye kuona kuwa ni wajibu kwa kila mwenye uwezo wa kufanya hivo. Wametumia hoja kwa udhahiri wa maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Enyi kongamano la mabarobaro! Yule miongoni mwenu atakayeweza kuoa basi na aoe. Kwani hilo litamfanya kuteremsha macho zaidi na kuhidhi utupu. Asiyeweza basi afunge. Kwani hiyo kwake ni kinga”

Wameipokea katika “as-Swahiyh” mbili kupitia kwa Ibn Mas´uud. Kisha wakataja kwamba kuoa ni sababu ya utajiri kwa kutumia dalili ya maneno Yake (Ta´ala):

إِن يَكُونُوا فُقَرَاءَ يُغْنِهِمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ

“Wakiwa mafakiri Allaah basi Atawatajirisha katika fadhila Zake.”

Wakataja kutoka kwa Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) kuwa amesema:

“Mtiini Allaah katika yale aliyokuamrisheni katika kuoa atakutimizieni yale aliyokuahidini katika utajiri. Amesema (Ta´ala):

إِن يَكُونُوا فُقَرَاءَ يُغْنِهِمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ

“Wakiwa mafakiri Allaah basi Atawatajirisha katika fadhila Zake.”

Ibn Mas´uud amesema:

“Tafuteni utajiri kwa kuoa. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِن يَكُونُوا فُقَرَاءَ يُغْنِهِمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ

“Wakiwa mafakiri Allaah basi Atawatajirisha katika fadhila Zake.”

Ameipokea Ibn Jariyr. al-Baghawiy pia amepokea mfano wake kutoka kwa ´Umar[3].

 Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Allaah (Subhaanah) akahalalisha kuoa, kuacha na kumuoa mwanamke aliyeachika baada ya kuolewa na mume wake mwingine. Manaswara wanaharamisha kuoana kati yao. Yule watayemuhalalishia kuoa hawamuhalalishii kuacha. Mayahudi wanahalalisha kuacha. Lakini wanaona kwamba mwanamke aliyeachwa akiolewa na mume mwingine anaharamika kwake. Manaswara hawana talaka. Mayahudi hawana jambo la kurejeana baada ya yule mume mwingine kumuoa. Allaah (Ta´ala) akawahalalishia wanawake waumini yote mawili.”[4]

Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema katika “al-Hadyi an-Nabawiy” akibainisha manufa ya jimaa ambayo ni moja katika makusudio ya ndoa:

“Jimaa kimsingi imewekwa kwa ajili ya mambo matatu ambayo ndio makusudio yake ya kimsingi:

1 – Kuhifadhi kizazi na kudumisha sampuli hiyo mpaka ikamilike ile eda ambayo Allaah ameikadiria kudhihiri kwake katika ulimwengu huu.

2 – Kuyatoa yale maji ambayo kuyazuia kunaudhuru ujumla wa mwili wa mtu.

3 – Kutekeleza ile haja, kupata ile ladha na kustareheka na neema.”[5]

[1] 30:21

[2] 24:32

[3] (05/94-95).

[4] (05/94-95) chapa ya Daar-ul-Andalus.

[5] (03/149).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 99-100
  • Imechapishwa: 18/11/2019