Tofauti kati ya unafiki mkubwa na unafiki mdogo:

1- Unafiki mkubwa unamtoa mtu nje ya Uislamu na unafiki mdogo haumtoi mtu nje ya Uislamu.

2- Unafiki mkubwa ni kutofautiana siri na anavyodhihirisha mtu katika kuamini na unafiki mdogo ni kutofautiana siri na anavyodhihirisha mtu katika matendo na si imani.

3- Unafiki mkubwa hautoki kwa muumini. Lakini unafiki mdogo unaweza kumtokea muumini.

4- Mara nyingi mwenye unafiki mkubwa hatubii. Iwapo atatubia wanachuoni wametofautiana juu ya hukumu ya kukubaliwa kwa tawbah. Hilo ni tofauti na unafiki mdogo. Mwenye nao anaweza kutubia kwa Allaah ambapo Allaah akamsamehe. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Ni mara nyingi muumini anaingiliwa na moja katika tanzu za unafiki kisha Allaah akamsamehe. Pengine wakati mwingine akaingiliwa na mambo yanayopelekea katika unafiki na Allaah akamzuilia nayo. Muumini hupewa mtihani kwa wasiwasi wa shaytwaan na wasiwasi wa kufuru inamyofanya kifua chake kuhisi dhiki. Maswahabah wamesema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika mmoja wetu anahisi ndani ya nafsi yake kitu ambacho kuporomoka kutoka mbinguni kunapendeza zaidi kwake kuliko kukitamka.” Akasema: “Hiyo ni imani ya wazi.” Katika upokezi mwingine imekuja: “… ambacho anakifanya kikubwa kukizungumza.” Akasema: “Himdi njema zote anastahiki Allaah ambaye amerudisha njama zake kwenda katika wasiwasi wake.”  Bi maana kufikia wasiwasi huu. Kukichukia kukubwa namna hii na kukizuia na moyo ni miongoni mwa mambo ya imani ya wazi.”[1]

Ama wenye unafiki mkubwa Allaah amesema juu yao:

صُمٌّ بُكْمٌ عُمْيٌ فَهُمْ لَا يَرْجِعُونَ

“Viziwi, mabubu, vipofu, basi hawatorejea.”[2]

Bi maana hawarudi katika Uislamu kwa ndani. Amesema (Ta´ala) juu yao:

أَوَلَا يَرَوْنَ أَنَّهُمْ يُفْتَنُونَ فِي كُلِّ عَامٍ مَّرَّةً أَوْ مَرَّتَيْنِ ثُمَّ لَا يَتُوبُونَ وَلَا هُمْ يَذَّكَّرُونَ

“Je, hawaoni kwamba wao wanatahiniwa katika kila mwaka mara moja au mara mbili; halafu hawatubii na wala wao hawakumbuki?”[3]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Wanachuoni wametofautiana juu ya kukubaliwa kwa tawbah yake kidhahiri. Hilo si kwa jengine isipokuwa ni kwa sababu halijulikani. Kwa sababu wao siku zote hudhihirisha Uislamu.”[4]

[1] Kitaab-ul-Iymaan, uk. 238.

[2] 02:18

[3] 09:126

[4] Majmuu´-ul-Fataawaa (28/434-435).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 93-94
  • Imechapishwa: 17/03/2020