Kuifanyia uvuaji katika imani maana yake ni mtu kusema:

“Mimi ni muumini Allaah akitaka.”

Watu wametofautiana katika maoni tatu:

1- Ni haramu kufanya uvuaji, haya ni maoni ya Murji-ah, Jahmiyyah na wengineo. Maoni haya yamejengeka juu ya kwamba imani ni kitu kimoja na ni kitu ambacho kila mtu anakitambua. Kwa vile imani ni kule kuthibitisha/kusadikisha kwa moyo, hivyo basi mtu akifanya uvuaji ina maana kwamba ana mashaka. Ndio maana wanawaita wale wenye kufanya uvuaji “wenye mashaka”.

2- Ulazima wa kufanya uvuaji. Maoni haya yamejengeka juu ya mambo mawili:

1- Imani ni ile ambayo mtu anakufa juu yake. Mtu anakuwa ima ni muumini au kafiri kwa kutegemea na ile hali aliyofiaemo. Hili ni jambo la huko mbeleni lisilojulikana. Hivyo haijuzu kukata kitu. Wengi katika Kullaabiyyah na wengineo waliokuja nyuma wanatumia hoja hii. Hata hivyo haijulikana kuwa kuna yeyote katika Salaf alitumia hoja hii. Hoja yao ilikuwa:

2- Imani isiyofungamana inapelekea kufanya yale mambo yote yaliyoamrishwa na kujiepusha na yale mambo yote yaliyokatazwa. Hiki ni kitu ambacho mtu hawezi kukikata juu ya nafsi yake. Endapo atafanya hivo, basi atakuwa amejisifia nafsi yake na amejishuhudia kuwa ni katika wachaji Allaah na watu wema. Katika hali hii anatakiwa vilevile kushuhudia kuwa ni katika watu wa Peponi, jambo ambalo ni malazimisho yasiyowezekana.

3- Msimamo wa kupambanua.

Ikiwa mtu anafanya uvuaji kwa sababu ana mashaka, ni jambo la haramu bali ni kufuru. Imani ni jambo la kukata na mashaka yanapingana nayo.

Ikiwa kufanya uvuaji kunatokana na mtu kuchelea kujisifu na kushuhudia kuwa imani yake imekamilika kwa maneno, vitendo na imani, basi kufanya uvuaji itakuwa ni lazima ili mtu asitumbukie katika makatazo haya.

Na ikiwa lengo ni kutafuta baraka na kubainisha sababu kwamba imani ya moyo inatokana na matakwa ya Allaah, jambo hili linafaa. Kuyashurutisha matakwa ya Allaah kwa njia hii haina maana kwamba imani haikuhakikishwa na kupatikana. Mazingira kama haya yametajwa katika mambo yaliyohakikishwa. Kwa mfano Allaah (Ta´al) amesema:

لَتَدْخُلُنَّ الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ إِن شَاء اللَّهُ آمِنِينَ مُحَلِّقِينَ رُؤُوسَكُمْ وَمُقَصِّرِينَ لَا تَخَافُونَ

“Bila shaka mtaingia Msikiti mtakatifu Allaah akitaka mkiwa hali ya kuwa na amani, wenye kunyoa vichwa vyenu na wenye kupunguza. Hakuna mnachoogopa!”

Hapa inapata kujulikana kuwa si sahihi kuhukumu uvuaji kwa njia ya kuachia. Bali ni lazima suala hili lifafanuliwe kutokana na njia iliyotajwa na Allaah ndiye anajua zaidi.

Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

08 Dhul-Qa´dah 1380.

Himdi zote njema ni stahiki ya Allaah ambaye kwa neema Zake yanatimia mambo mema

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 97-98
  • Imechapishwa: 15/05/2020