1 – Ibn ´Umar amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinishika mabega yangu akasema: “Ishi duniani kama vile mgeni au mpita njia.”

Hakuna mashaka juu ya usahihi wake.

2 – Katika Hadiyth hii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemwamrisha Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kuishi duniani kama mgeni au mpita njia. Ni kana kwamba anamwamrisha kukinaika na kichache. Kwa sababu pindi mgeni na msafiri wanapokuwa mbali na nyumba zao hawalengi kufikia utajiri wowote. Hupendelea kukinaika na kidogo kuliko kukithirisha vingi vya duniani.

3 – Aktham bin Swayfiy amesema:

“Ee mwanangu kipenzi! Anayekata tamaa juu ya kilichompita anajichosha mwili wake. Anayetosheka na yale alionayo basi daima hufurahi.”

4 – Ibn Mas´uud amesema:

“Mambo matatu yamekwishakadiriwa na hakuna yeyote ambaye atachuma zaidi ya mwengine; uumbaji, tabia, riziki na muda wa kuishi.”

5 – Miongoni mwa zawadi kubwa ambazo Allaah huwapa waja Wake ni kukinaika. Hakuna kitu kinachoupumzisha mwili zaidi kama kuridhia makadirio na kutegemea ugawanyo wa Allaah wa riziki. Kama kukinaika kusingelikuwa na sifa nyingine nzuri isipokuwa kupumzisha mwili na kuulinda kuingia maeneo mabaya kwa ajili ya kutafuta cha ziada, basi ingelikuwa ni lazima kwa mwenye busara daima kuwa mwenye kukinaika.

6 – Muhammad bin al-Munkadir amesema:

“Kukinaika ni mali isiyokwisha.”

7 – Mwenye busara anatambua kwamba asiyekuwa na kukinaika basi mali haitomzidishia utajiri. Bora kuwa na pesa kidogo na simanzi ndogo kuliko kuwa na pesa nyingi na tabu nyingi. Mwenye busara hulipa kisasi juu ya bidii ya kukinaika kama ambavo hulipa kisasi kwa adui kwa adhabu. Kile kinachozuia riziki ya mwenye busara ndio kinachomfanya mjinga kupata riziki.

8 – Ibn-ul-Mubaarak amesema:

“Muruwa wa kukinaika ni mzuri kuliko muruwa wa kutoa.”

9 – Kukinaika kunakuwa moyoni. Anayekinaika moyo wake hukinaika mikono yake. Ambaye umefukarika moyo wake basi hautomfaa kitu utajiri wake. Mwenye kukinaika hatokasirika. Ataishi akiwa na amani na utulivu. Asiyekinaika kamwe haishi kutamani yale yaliyompita. Ni kana vile utajiri na umasikini vinashindana kati ya waja.

10 – al-Madiyniy amesema:

“Subira kwa njia ya kujizuia na kukinaika wakati wa haja na umasikini ni matukufu zaidi kuliko kutoa.”

11 – Yule anayepambana na nafsi yake juu ya kukinaika kisha akawahusudu watu kwa yale walionayo hayo si kutokana na kukinaika wala ukarimu – bali ni kutokana na kushindwa na kutofaulu.

12 – Muhammad bin Ka´b al-Quradhwiy amesema juu ya maneno Yake (Ta´ala):

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً

“Mwenye kutenda mema katika wanamume au wanawake – ilihali ni muumini – basi Tutamhuisha maisha mazuri.”[1]

 “Bi maana kukinaika.”

[1] 16:97

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 148-153
  • Imechapishwa: 10/08/2021