Swali: Baadhi ya watu katika kijiji chetu huleta kikosi cha Mashaykh miongoni mwa wale wenye elimu ya kusoma Qur-aan ambapo wanasoma Qur-aan kwa hoja kuwa Qur-aan hii inamfaa maiti na inamrehemu. Wengine wanamwalika Shaykh au wawili kwa ajili ya kusoma Qur-aan juu ya kaburi la huyu maiti. Wako wengine wanafanya sherehe kubwa ambapo wanamwalika mmoja katika wasomaji wanaotambulika kupitia kipaza sauti kwa ajili ya kuhuisha kumbukumbu ya kila mwaka kwa ajili ya kule kufa kwa yule mpendwa wao. Ni ipi hukumu ya dini juu ya hilo? Kisomo cha Qur-aan kinamfaa yule maiti kwenye kaburi au kwenginepo? Ni ipi njia bora ya kumfaa yule maiti?

Jibu: Hichi kitendo ni Bid´ah na hakijuzu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[1]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[2]

 Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Zipo Hadiyth nyingi zenye maana kama hii.

Haikuwa ni miongoni mwa Sunnah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala miongoni mwa Sunnah za makhaliyfah wake waongofu (Radhiya Allaahu ´anhum) kusoma juu ya makaburi, kusherehekea wafu na ukumbusho wa kifo chao. Kheri zote zinapatikana kwa kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), makhaliyfah wake na wale watakaofata njia yao. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Wale waliotangulia mwanzoni ambao ni Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye na amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito – ni wenye kudumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza baada yangu. Shikamaneni nazo barabarab na ziumeni kwa magego. Nakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa. Kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotofu.”[4]

Vilevile imsihi kutoka kwamba kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alikuwa anasema katika Khutbah ya ijumaa:

“Amma ba´d: Hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Allaah na uongofu bora ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa na kila Bid´ah ni upotevu.”[5]

Zipo Hadiyth nyingi zenye maana kama hii.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameweka wazi katika Hadiyth ambazo ni Swahiyh yale yanayomnufaisha muislamu baada ya kufa kwake. Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Anapofariki mwanadamu basi matendo yake hukatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu ambayo watu wananufaika nayo au mtoto mwema mwenye kumuombea du´aa.”[6]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Aliulizwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mtu mmoja na akasema:

“Ee Mtume wa Allaah! Kuna chochote kilichobaki katika haki juu ya wazazi wangu naweza kuwafanyia baada ya kufa kwao?” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ndio, kuwaombea du´aa, kuwaombea msamaha, kutekeleza ahadi zao baada yao, kuwakirimu marafiki zao na kuwaunga jamaa zao ambao hawaungiki isipokuwa kwao.”[7]

Makusudio ya ´ahadi` ni wasia ambao ameacha anausia yule maiti. Miongoni mwa kuwatendea wema ni kuutekeleza ikiwa unaafikiana na Shari´ah takasifu. Miongoni mwa kuwatendea wema wazazi ni kuwatolea swadaqah, kuwaombea du´aa, kuwahijia na kuwafanyia ´Umrah.

[1] Muslim (1718).

[2] Muslim (1718).

[3] 09:100

[4] Ahmad (16694), Abu Daawuud (4607) na Ibn Maajah (46).

[5] Muslim (867).

[6] Muslim (1631).

[7] Ahmad (15629), Abu Daawuud (5142) na Ibn Maajah (3664).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 130-132
  • Imechapishwa: 21/07/2022