38. Kuwafanyia maulidi waliyomo ndani ya makaburi

Swali: Katika kijiji chetu kuna kaburi la mmoja katika watu wema. Watu wanamwendea na wanamtangulizia nadhiri na vichinjwa. Wanalizunguka kaburi na kulipapasapapasa kwa ajili ya kutafuta baraka. Hufanya hapo kwake duara za Dhikr. Yote hayo yanafanyika pamoja na mchanganyiko wa wanamme na wanawake. Sambamba na hilo wanamwita yule aliyemo ndani ya kaburi, kutaka uokozi kwake na kutaka msaada kutoka kwake. Ni ipi hukumu kwa watu hawa na juu ya matendo yao haya? Ni ipi hukumu ya maulidi anayofanyiwa Shaykh huyu na wengine?

Jibu: Ambaye anayaenda makaburi ya waliokufa na kuwaomba, kuwataka kuwaponya wagonjwa, akaomba uokozi kutoka kwao, msaada, kuingia Pepo, kusalimika na Moto, kuwawekea nadhiri, akawachinjia, akatufu makaburi yao kwa ajili ya kutafuta baraka na malipo kutoka kwao, kusalimika kutokamana na Moto, kuyaponya magonjwa, kukunjuliwa riziki au mfano wa hayo, yote hayo ni ukafiri na shirki kubwa. Hii ni dini ya washirikina. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[1]

Amesema (Subhaanah) kuhusu masanamu na wale wengine wote wanaoabudiwa badala ya Allaah:

إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ ۚ وَلَا يُنَبِّئُكَ مِثْلُ خَبِيرٍ

”Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu, na hata wakisikia, hawatakuitikieni na siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wenu na wala hakuna atakayekujulisha vyema kama Mwenye khabari zote za ndani.”[2]

Ameita kuwa ni shirki.

Amesema (Subhaanah):

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote yule anayeomba pamoja na Allaah mungu mwengine – hana ushahidi wa wazi juu ya hilo – basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake. Hakika hawafaulu makafiri.”[3]

Kitendo cha kumwomba asiyekuwa Allaah ameita kuwa ni ukafiri, upotofu na shirki.

Vivyo hivyo kufanya Adhkaar na maulidi kwenye makaburi ni Bid´ah. Kufanya sherehe karibu na kaburi, maulidi, Adhkaar, duara za kielimu au Qur-aan mambo haya ni Bid´ah na sio shirki. Kuhusu kuwaomba mahitaji kutoka kwao na kupapasapapasa mchanga wa kaburi kwa ajili ya kutafuta baraka, kuwaomba wakuponyee wagonjwa ni katika ukafiri mkubwa. Tunamuomba Allaah afya na hapana ndugu na uwezo isipokuwa kwa msaada wa Allaah.

Kuhusu maulidi yote ni Bid´ah. Kusherehekea maulidi yote hayo ni Bid´ah kwa mujibu wa wanazuoni wakaguzi. Kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hakutuwekea Shari´ah ya jambo hilo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakusherehekea mazazi yake. Vivyo hivyo Maswahabah hawakusherehekea mazazi yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), mazazi ya Abu Bakr, mazazi ya ´Umar, mazazi ya ´Uthmaan wala mazazi ya ´Aliy. Wao ndio viigizi na wabora. Endapo mambo hayo yangelikuwa ni kheri basi wangelitutangulia kwayo. Kwa hivyo kusherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ya Mashaykh, ya viongozi au ya wengine yote ni Bid´ah na yote hayajuzu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayezua kitendo kisichokuwa katika amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[4]

Vilevile amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[5]

Amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nakutahadharisheni na mambo yaliyozuliwa. Kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotofu.”[6]

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema katika Khutbah ya ijumaa:

“Amma ba´d: Hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Allaah na uongofu bora ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa na kila Bid´ah ni upotevu.”[7]

Kwa hivyo ni lazima kwa waislamu kutahadhari na Bid´ah hizi na wajiepushe nazo mbali. Ikiwa yako na mchanganyiko kati ya wanamme na wanawake basi jambo linakuwa kubwa zaidi, mtihani unakuwa mkubwa zaidi na dhambi zinakuwa nyingi zaidi. Kwa sababu kuchanganyikana kati ya wanamme na wanawake kwenye kaburi au katika sherehe yoyote ni maovu. Aidha ni miongoni mwa sababu za uzinzi, machafu na ni miongoni mwa sababu zinazopelekea kutumbukia katika mambo ya haramu. Ni lazima kutahadhari na jambo hilo hata kama si sherehe. Hata katika karamu nyingine haijuzu kwa wanamme wakachanganyikana na wanawake katika sherehe na wakachanganyikana katika sherehe ya harusi au sherehe yoyote ile. Kwa sababu jambo hilo linasababisha wanamme kufitinika na wanawake na kinyume chake. Kwa hivyo ni lazima kuwatenganisha na mkusanyiko wa wanawake uwe upande wao na mkusanyiko wa wanamme uwe upande wao katika karamu, sherehe zinazofaa kama mfano wa harusi na nyenginezo.

[1] 72:18

[2] 35:14

[3] 23:117

[4] al-Bukhaariy (2697) na Muslim (1718).

[5] Muslim (1718).

[6] Ahmad (16694), Abu Daawuud (4607) na Ibn Maajah (46).

[7] Muslim (867).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 126-129
  • Imechapishwa: 20/07/2022