Swali: Kuna mtu mmoja amefariki mjini kwetu na tukafikiwa na khabari za kufa kwake mida ya mchana na tukawaona wanawake vikongwe wa mji wakienda nyumbani kwake. Baada ya kumvika sanda akalazwa katikati ya wanawake na wao wanawake wamemzunguka. Tukawauliza sababu ya wao kumwendea wakasema ni kwa sababu ya kutafuta baraka kwake. Ni ipi hukumu ya matendo yao haya? Je, ni Sunnah?

Jibu: Kitendo hichi hakijuzu. Bali ni maovu. Kwa sababu haijuzu kwa yeyote kutafuta baraka kwa waliokufa au makaburi au wala kuwaomba badala ya Allaah na akawaomba kuwatatulia haja, kuwaponya wagonjwa au mfano wa mambo hayo. Kwa sababu ´ibaadah ni haki ya Allaah pekee na kunaingia vilevile kule kutafuta baraka. Yeye (Subhaanah) ndiye Mwenye kusifiwa kubariki. Amesema (´Azza wa Jall) katika Suurah “al-Furqaan”:

تَبَارَكَ الَّذِي نَزَّلَ الْفُرْقَانَ عَلَى عَبْدِهِ لِيَكُونَ لِلْعَالَمِينَ نَذِيرًا

“Amebarikika Yule ambaye ameteremsha Pambanuzi kwa mja Wake ili awe ni muonyaji kwa walimwengu.”[1]

تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ

”Amebarikika Ambaye mkononi Mwake umo ufalme.”[2]

Maana yake ni kwamba Yeye (Subhaahah) amefikia kilele cha mwisho katika utukufu na baraka.

Kuhusu kiumbe yeye ni mwenye kubarikiwa akiongozwa, akatengenezwa na Allaah na akawanufaisha viumbe. Allaah (´Azza wa Jall) amesema kuhusu mja na Mtume Wake ´Iysaa mwana wa Maryam (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

قَالَ إِنِّي عَبْدُ اللَّـهِ آتَانِيَ الْكِتَابَ وَجَعَلَنِي نَبِيًّا وَجَعَلَنِي مُبَارَكًا أَيْنَ مَا كُنتُ وَأَوْصَانِي بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ مَا دُمْتُ حَيًّا

“Akasema: “Hakika mimi ni mja wa Allaah; amenipa Kitabu na amenifanya kuwa Nabii na amenifanya kuwa mwenye kubarikiwa popote nitakapokuweko na ameniusia swalah na zakaah muda wa kuwa niko katika uhai.”[3]

[1] 25:01

[2] 67:01

[3] 19:30-31

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 124-125
  • Imechapishwa: 19/07/2022