36. Kuamini kuteremka kwa ´Iysaa


Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inatakiwa kuamini kuwa ´Iysaa bin Maryam (´alayhis-Salaam) atashuka na kumuua karibu na mlango wa Ludd.”

MAELEZO

Haya yamethibiti katika Hadiyth Swahiyh katika “as-Swahiyh” ya Muslim[1]. Imetajwa namna ambavyo ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anavyoshuka na mikono ikiwa juu ya mbawa za Malaika wawili. Atakuwa na shuka mbili zilizopakwa rangi ya zafarani na manjano na atashuka kwenye mnara wa Dameski. Waislamu wajiunge naye na kutokea hapo ndipo ataenda kwa ad-Dajjaal na kumuua.

al-Masiyh huyu ambaye ni Nabii na ambaye ni Mtume ndiye ambaye atamuua al-Masiyh ad-Dajjaal. ´Iysaa ameitwa al-Masiyh kwa sababu ya kusafiri kwake, ad-Dajjaal ameitwa al-Masiyh kwa sababu jicho lake limefutwa. ´Iysaa ni Nabii na Mtume, ad-Dajjaal ni mwongo na mdanganyi. Allaah atamfanya al-Masiyh ´Iysaa bin Maryam (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuua al-Masiyh huyu wa uongo.

Baada ya (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuua ndipo atajitokeza Ya´juuj na Ma´juuj. Wakati huo ndio ´Iysaa na waumini wataenda kwenye mlima wa Twuur. ´Iysaa na waumini watamuomba Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amuangamize Ya´juuj na Ma´juuj na Allaah afanye hivo. Ndipo ardhi ianze kutoa harufu mbaya kwa sababu ya miili yao iliyokufa ambapo wamuombe Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) awatokomeze. Ndipo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ataagiza ndege zilizo kubwa kama shingo za ngamia zichukue wafu hao na kuwatupa kule ambako Allaah anataka. Allaah atafanya kunyeshe mvua kubwa ambapo ardhi itakuwa kama kio kisafi. Halafu Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) aamrishe ardhi ilete baraka zake mpaka kundi zima la watu lile kutoka kwenye mkomamangu mmoja na kusimama chini ya kivuli chake. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) atayabariki vilevile maziwa mpaka kundi la watu linywe maziwa ya ngamia na maziwa ya ng´ombe na mpaka kabila zima linywe maziwa ya mbuzi. Ni baraka kutoka kwa Allaah. Baada ya hapo Allaah atume upepo mzuri kwa watu wa ´Iysaa na wafe. Baada ya hapo hakuna wataobaki katika ardhi isipokuwa tu viumbe waovu kabisa. Wataishi bila mpangilio kama punda. Qiyaamah kitawasimamia watu hawa.

Hizi ni baadhi ya alama kubwa za Qiyaamah: kujitokeza kwa ad-Dajjaal, kushuka kwa ´Iysaa, kujitokeza kwa mnyama na jua kuchomoza kutoka magharibi. Yote haya yatatokea na ni miongoni mwa alama kubwa za Qiyaamah.

[1] Muslim (2937).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 404-405
  • Imechapishwa: 25/09/2017