32. Khitimisho ya kitabu “ad-Dimaa’ at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa'”

Mpaka hapa inaisha mada muhimu ambayo nimetaka kuiandika. Nimekomeka na misingi na vidhibiti vya masuala haya. Vinginevyo matawi ya maudhui hii, upambanuzi na mambo yanayomtokea mwanamke ni bahari isiyokuwa na mwisho. Lakini hata hivyo yule mwenye uoni wa mbali anaweza kuyarudisha mambo katika misingi na upambanuzi wa vidhibiti na kuleta uwiano kati yayo.

Mtu ambaye anajibu maswali anatakiwa atambue kuwa yeye ni mpatanishi kati ya Allaah na viumbe Vyake inapokuja katika kufikisha na kuwabainisha ujumbe uliokuja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba ataulizwa juu ya yale yaliyomo katika Qur-aan na Sunnah. Qur-aan na Sunnah ndio chemchem mbili ambazo mja amepewa kama kazi kuzifahamu na kuzitendea kazi. Kila kinachoenda kinyume na Qur-aan na Sunnah ni kosa linalotakiwa kurudishwa kwa mwenye nalo. Haijuzu kutendea kazi kosa hilo hata kama yule mwenye maoni hayo anapewa udhuru katika Ijtihaad yake. Analipwa kwa Ijtihaad yake, lakini hata hivyo haitakiwi kufanyia kazi kosa lake.

Ni wajibu kwa mwenye kujibu maswali amtakasie nia Allaah (Ta´ala) na kumtaka msaada katika kila tokeo linalotokea na kumuomba (Ta´ala) uthibitisho na uafikisho katika usawa.

Anayejibu maswali anatakiwa kuangalia yaliyomo katika Qur-aan na Sunnah. Aangalie na kufanya utafiti kutoka kwavyo na kuchukua msaada kutoka katika maneno ya wanachuoni katika kuifahamu Qur-aan na Sunnah. Ni jambo linalotokea mara nyingi kunazuka jambo fulani ambapo mtu anafanya utafiti kiasi na anavyoweza na hatimae anapata jibu kutoka katika maneno ya wanachuoni. Wakati fulani hapati jibu analohisi utulivu kwalo, na wakati mwingine huenda asipate jibu kabisa. Upande mwingine akirejea katika Qur-aan na Sunnah anapata hukumu ilio karibu na ya wazi, yote hayo yanatokamana na Ikhlaasw ya mtu, elimu na uelewa.

Mtu anayejibu maswali anapaswa kufanya utulivu na asiwe na haraka wakati hukumu ni yenye kutia mashaka. Ni mara ngapi mtu hufanya haraka, kisha baada ya uchunguzi wa karibu, inakuja kumbainikia kuwa alikosea! Kwa ajili hiyo anakuwa ni mwenye kujuta na anashindwa kukabiliana na kosa alilofanya.

Watu wakijua kuwa mtu anayejibu maswali ni mwangalifu na anathibitisha kwanza kabla ya kujibu, wanakuwa ni wenye kuamini majibu yake na kuyapokea. Upande mwingine wakiona kuwa ni mwenye haraka – na wenye haraka hukosea mara nyingi – hawatoamini majibu yake. Hivyo haraka zake na kosa lake inakuwa ni sababu ya kujinyima mwenyewe na wengine elimu na usawa wa aliyomo.

Ninamuomba Allaah (Ta´al) atuongoze sisi na ndugu zetu waislamu katika njia iliyonyooka na atuangalie kwa uangalizi na ulinzi Wake na atukinge na makosa. Hakika Yeye ni mwingi wa kutoa na Mkarimu. Swalah na zalaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote. Sifa njema ni za Allaah ambaye kwa neema yake yanatimia mambo mema.

Imeandikwa na mja fakiri kwa Allaah Muhammad bin Swaalih al-´Uthaymiyn

Mida ya asubuhi tarehe 14 Sha´baan 1392

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Dimaa’ at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa’ http://www.ibnothaimeen.com/all/books/article
  • Imechapishwa: 30/10/2016