Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msingi wa pili ni kuijua dini ya Kiislamu kwa dalili. Nako ni kujisalimisha kwa Allaah kwa Tawhiyd, kunyenyekea Kwake kwa kumtii na kujitenga mbali na Shirki na watu wake. Hili lina daraja tatu: Uislamu, Imani na Ihsaan. Kila daraja ina nguzo zake.

MAELEZO

Huu ndio msingi wa pili; kuijua dini ya Kiislamu. Uislamu una ngazi tatu zilizobainishwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ngazi ya kwanza ni Uislamu. Uislamu maana yake ni kumtakasia ´ibaadah Allaah pekee. Uislamu ni kujisalimisha kwa Allaah kwa ´ibaadah. Kumkhusisia nayo Yeye pasi na wengine wote. Aidha inatakiwa kujitenga mbali na shirki na watu wake.

Pindi mja atapohakikisha hayo atakuwa amesilimu kwa njia ya kwamba amenyenyekea na kumdhalilikia Allaah peke yake kwa ´ibaadah na kujitenga mbali na shirki na watu wake. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ

“Basi atakayemkanusha twaaghuut na akamwamini Allaah kwa hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika.” (02:256)

Kukufuru Twaaghuut ina maana mtu kujitenga mbali na shirki na watu wake, kuyakemea hayo na kuonelea kuwa ni batili.

Kuna vilevile ngazi ya imani na Ihsaan. Zote zinaingia katika dini ya Uislamu. Hii ndio dini ambayo Allaah amewawekea kwayo Shari´ah waja Wake na akawatuma kwayo Mitume Wake wote. Ngazi ya Uislamu imekusanya yale matendo ya dhahiri.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 39-40
  • Imechapishwa: 05/01/2017