27. Khitimisho ya kitabu “al-Hijaab”

Nimeiingilia mada hii kwa undani kwa sababu watu wana haja ya kuwa na ujuzi kuhusu suala hili kubwa na la kijamii. Wengi ambao wanataka wanawake waoneshe nyuso zao hawakulifanyia suala hili utafiti na uhakiki utakikanao. Ni wajibu kwa kila mtafiti kuwa mwadilifu na mwenye inswafu, asizungumze kabla ya kujifunza na asimame katika maoni ya dalili tofauti msimamo wa hakimu aliye kati ya watu wawili; asiwe ni mwenye kupendelea na ahukumu kwa elimu. Asichague upande bila ya dalili yake. Aangalie dalili za pande zote na asisukumwe na mtazamo ambao tayari kishakuwa nao mpaka akapetuka na kuvuka mipaka dalili zake na akafikia mpaka kupuuza na kufanya si lolote si chochote dalili za upande mwingine. Ndio maana wanachuoni wanasema inatakikana kwa mtu kustadili kabla ya [kuanza] kuonelea. Hili ni kwa sababu maoneleo yanatakiwa kuwa chini ya dalili na si kinyume chake. Ambaye anaonelea kabla ya dalili anakuja kuathirika na maoneleo yake ambayo yanamfanya ima kupitilia mbali maandiko yasiyomsapoti au kuyapotosha ikiwa hakuweza kuyatupilia mbali.

Mimi na wengine sote tumeona jinsi kutafuta dalili juu ya maoneleo kunavodhuru. Hilo humfanya mtu ikiwa ni pamoja na Hadiyth dhaifu kuonelea kuwa ni Swahiyh na kufasiri maandiko kwa njia zote ziwezekanazo ili tu kuyathibitisha maoni yake. Nilisoma makala ya mwandishi mmoja ambaye alitumia hoja Hadiyth ya ´Aaishah jinsi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivomwambia Asmaa´ bint Abi Bakr (Radhiya Allaahu ´anhum):

“Ee Asmaa´! Wakati mwanamke anapobaleghe hatakiwi kuonesha chochote isipokuwa hiki na hiki” na akaashiria uso na vitanga vyake vya mikono.”

Hadiyth imepokelewa na Abu Daawuud. Mwandishi huyo amesema kuwa wanachuoni [wote] wamekubaliana juu ya kwamba Hadiyth ni Swahiyh. Si kweli. Ni vipi watakubaliana na wakati Abu Daawuud mwenyewe amesema kuwa kasoro ya Hadiyth kuna mkato katika mnyororo na Ahmad na maimamu wengine wamesema kuwa mpokezi mmoja ni dhaifu? Ushabiki na ujinga unamfanya mtu kutumbukia kwenye mtihani na maangamio. Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

Vua mavazi mawili

yanayomfanya yule mvaaji kudharauliwa na kudhalilishwa

Vazi lililokusanya ujinga

na juu yake kuna ushabiki – ubaya uliyoje wa vazi hili!

Jivishe uadilifu, nguo iliyo na fakhari zaidi

ambayo haijapatayo kuketi kwa mtu

Waandishi na watunzi wanapaswa kuhadhari kupuuza na kutelekeza dalili na kuwa na haraka ya kuzungumza pasina elimu na hivyo wakawa ni wenye kutumbukia katika wale ambao Allaah (Ta´ala) amesema:

فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا لِّيُضِلَّ النَّاسَ بِغَيْرِ عِلْمٍ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ

“Nani dhalimu zaidi kuliko yute anayemzulia Allaah uongo ili apoteze watu bila elimu? Hakika Allaah Hawaongozi watu madhalimu.”[1]

Vilevile asipuuzie dalili na kukadhibisha yenye kutolewa dalili ikawa ni shari chungumzima na akaja kutumbukia katika wale ambao Allaah (Ta´ala) amesema:

فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن كَذَبَ عَلَى اللَّـهِ وَكَذَّبَ بِالصِّدْقِ إِذْ جَاءَهُ ۚأَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْكَافِرِينَ

“Basi ni nani dhalimu zaidi kuliko yule aliyemsingizia uongo Allaah na akaukadhibisha ukweli ulipomjia? Je, kwani [Moto wa] Jahannam si makazi kwa makafiri?”[2]

Ninamuomba Allaah (Ta´ala) atuoneshe haki na atuwafikishe kuweza kuifuata na atuoneshe batili na atuwafikishe kuweza kujiepusha nayo na atuongoze katika njia iliyonyooka. Hakika Yeye ni mwingi wa kutoa na Mkarimu. Allaah amsifu, ambariki na kumswalia Mtume wetu Muhammad, familia yake na Maswahabah zake wote.

Imeandikwa na Muhammad bin Swaalih al-´Uthaymiyn

[1] 06:144

[2] 39:32

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hijaab, uk. 34-37
  • Imechapishwa: 26/03/2017