25. Kuamini matukio baada ya kifo na yale yote yenye maana hiyo

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“… na kwamba ummah huu utapewa mtihani katika makaburi yao. Wataulizwa juu ya imani na Uislamu na ni Mola na Mtume wao? Munkar na Nakiyr watamwendea yule maiti kama anavyotaka Allaah (´Azza wa Jall). Yanatakiwa kuaminiwa na kusadikishwa”

MAELEZO

Maswali ya Munkar na Nakiyr ni jambo limethibiti katika Hadiyth ya al-Baraa´ bin ´Aazib (Radhiya Allaahu ´anh) na wengineo. Pindi mja anapofariki na akalazwa ndani ya kaburi hujiwa na Malaika wawili. Mmoja wao anaitwa Munkari na mwengine anaitwa Nakiyr. Watamuuliza yule maiti: “Ni nani Mola wako? Ni nani Mtume wako? Ni ipi dini yako?” Atasema: “Allaah ndiye Mola wangu, Uislamu ndio dini yangu na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio Mtume wangu.” Ndipo ataambiwa: “Tunakutambua. Hakika ulikuwa muumini. Lala kama ulikuwa muumini.” Ataonyeshwa sehemu yake Motoni iwapo angelikuwa kafiri. Kisha kutasemwa: “Allaah amekupa badala yake mahali Peponi.” Atasema: “Ee Mola wangu! Simamisha Qiyaamah! ambapo ataambiwa: “Subiri.” Malaika hao wawili watamwendea pia kafiri na kusema: “Ni nani Mola wako? Ni nani Mtume wako? Ni ipi dini yako?” Atasema: “Aah, sijui. Niliwasikia watu wakisema kitu nami nikakisema.” Halafu atapigwa nyundo. Lau nyundo hiyo ingepigwa kwenye mlima basi ungelisambuka na kugeuka udongo. Atapiga ulele kwa sauti ya juu mpaka viumbe wote watamsikia isipokuwa tu majini na watu. Endapo majini na watu wangelimsikia basi wangelikufa[1]. Hii ni sehemu tu ya adhabu ya ndani ya kaburi.”

[1] ´Abdur-Razzaaq (6737), Abu Daawuud (4751), al-Bukhaariy (1338) na Muslim (2870).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 116-118
  • Imechapishwa: 23/04/2019