Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inatakiwa kuamini uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)… “

MAELEZO

Kumekuja Hadiyth zilizopokelewa kwa njia nyingi kuhusu uombezi huko Aakhirah. Kutakuwepo uombezi aina saba. Tatu ni kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na nne ni kwa watu wote.

Uombezi ambao ni maalum kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pekee ni:

1- Uombezi ili watu wahukumiwe. Hiki ndio cheo chenye kusifiwa ambacho wale Mitume bora watajiepusha nacho. Nabii wa mwisho ambaye ataulizwa ni Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo atasema:

“Mimi ndiye mwenye kukistahiki, mimi ndiye mwenye kukistahiki.”[1]

2- Uombezi ili ifunguliwe Pepo[2].

3- Uombezi kwa ami yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Abu Twaalib ili akhafifishiwe adhabu[3]. Hakuna mwingine zaidi ya Abu Twaalib ambaye atapata uombezi huu.

Ama kuhusu nyombezi zengine, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atashirikiana na Mitume na Manabii wengine, wakweli, mashahidi na waumini wengine. Nyombezi zengine hizo ni:

1- Uombezi kwa watu wenye kustahiki kuadhibiwa kwa sababu ya madhambi yao. Wataombewa ili wasiadhibiwe na ili waingie Peponi pasi na adhabu.

2- Uombezi kwa watu walioingia Motoni kwa sababu ya madhambi yao. Wataombewa ili watoke Motoni na waingie Peponi.

3- Uombezi kwa watu walio na daraja za chini. Wataombewa ili zinyanyuliwe daraja zao ambazo hawastahiki. Ni fadhilah kutoka kwa Allaah.

4- Uombezi kwa watu walio kati ya Pepo na Moto kwa sababu matendo yao mwema yamekuwa sawa na matendo yao maovu. Matendo yao mema yamewazuia kuingia Motoni na maovu yao yamewazuia kuingia Peponi. Wataombewa ili Allaah awasamehe na waingie Peponi.

Nyombezi zote hizi zimethibiti kupitia Hadiyth zilizopokelewa kwa njia nyingi.

[1] al-Bukhaariy (4476) na Muslim (193).

[2] at-Tirmidhiy (3148). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (3543).

[3] al-Bukhaariy (6564) na Muslim (210).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 121-122
  • Imechapishwa: 23/04/2019