6- Kufa kwa tauni. Zipo Hadiyth kadhaa kuhusiana na jambo hilo:

A- Hafswah bint Siyriyn ameeleza: “Anas bin Maalik alinambia: “Yahyaa bin Abiy ´Amrah?” Nikasema: “Kwa tauni.” Akasema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kufa kwa tauni ni kufa shahidi kwa kila muislamu.”

Ameipokea al-Bukhaariy (10/156-157), at-Twayaalisiy (2113), Ahmad (03/150, 220, 223, 258-265).

B- ´Aaishah amesimulia kwamba alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu tauni ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamukhabarisha:

“Hiyo inakuwa ni adhabu ya Allaah anayoiagiza kwa amtakaye ambapo Allaah akaifanya kuwa ni rehema kwa waumini. Hakuna mja wowote atakayekutana na msimu wa tauni ambapo akabaki katika mji wake hali ya kuwa ni mwenye subira na akitambua kwamba hakuna kitachomfika isipokuwa kile alichoandikiwa na Allaah isipokuwa atakuwa na mfano wa ujira wa shahidi.”

Ameipokea al-Bukhaariy (10/157-158), al-Bayhaqiy (03/376), Ahmad (06/64, 145 na 252).

C- “Mashahidi na wale waliofishwa kwa tauni watakuja siku ya Qiyaamah na waliokufa kwa tauni watasema: “Sisi ni mashahidi.” Isemwe: “Watazameni; ikiwa majeraha yao ni kama ya mashahidi yanachuruzika damu na yenye harufu nzuri ya misiki, basi hao ni mashahidi.” Hatimaye wawapate wako hivo.”

Ameipokea Imaam Ahmad (04/185), at-Twabaraaniy katika “al-Kabiyr” (Majma 06/55/02) kwa cheni ya wapokezi nzuri kama alivosema al-Haafidhw (10/159) kupitia kwa ´Utbah bin ´Abdus-Sulamiy (Radhiya Allaahu ´anh). Inayo ushahidi kupitia kwa Hadiyth ya al-´Irbaadhw bin Saariyah (Radhiya Allaahu ´anh) ambayo imepokelewa na an-Nasaa´iy (02/63), Ahmad (04/128 na 129), at-Twabaraaniy (02/73) na al-Haafidhw pia ameifanya kuwa nzuri. Ni nzuri katika shawaahid.

Katika maudhui haya ipo Hadiyth kutoka kwa Abu Hurayrah na imekwishatangulia katika “alama ya tano” Hadiyth ya kwanza. Vilevile itakuja katika “alama ya nane na ya tisa” kupitia kwa ´Ubaadah na itakuja katika “alama ya kumi”.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 51-53
  • Imechapishwa: 02/02/2020