23. Sharti ya pili na ya tatu ya Shahaadah: Yakini na kuikubali


2- Sharti ya pili: Yakini. Mtamkaji awe na yakini juu ya yale yanayofahamishwa nalo. Haitomfaa kitu iwapo atakuwa na mashaka juu ya yale yanayofahamishwa nalo. Amesema (Ta´ala):

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا

“Hakika waumini ni wale waliomuamini Allaah na Mtume Wake kisha wakawa si wenye shaka.”[1]

Akiwa ni mwenye mashaka basi anakuwa mnafiki. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Utakayekutana naye nyuma ya ukuta huu anashuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah hali ya kuwa moyo wake ni wenye yakini basi mbashirie Pepo.”[2]

Ambaye moyo wake utakuwa si wenye yakini hatostahiki kuingia Peponi.

3- Sharti ya tatu: Kuikubali yale yanayopelekea katika neno hilo katika kumwabudu Allaah pekee yake na kuacha kuabudu vyengine asiyekuwa Yeye. Mwenye kulitamka na asiyakubali hayo na asilazimiane nalo, basi atakuwa ni miongoni mwa wale ambao Allaah amesema juu yao:

إِنَّهُمْ كَانُوا إِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ يَسْتَكْبِرُونَ وَيَقُولُونَ أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَّجْنُونٍ

“Hakika wao walipokuwa wakiambiwa ´hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah` hufanya kiburi na wanasema: “Je, hivi kweli sisi tuache waabudiwa wetu kwa ajili ya mshairi mwendawazimu?”[3]

Hii ni kama hali ya waabudu makaburi wa leo. Utawaona wanasema kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah lakini hata hivyo hawaachi kuyaabudu makaburi. Kwa hivyo si wenye kukubali maana ya “Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah”.

[1] 49:15

[2] Muslim (146).

[3] 37:35-36

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 48-49
  • Imechapishwa: 12/02/2020