21. Tofauti ya Salaf juu ya Tarawiyh na Witr


as-Salaf as-Swaalih wametofautiana juu ya idadi ya Rak´ah katika swalah ya Tarawiyh na Witr zikiswaliwa kwa pamoja. Kuna maoni ya wenye kusema ni Rak´ah kumi na moja. Kuna maoni ya wenye kusema ni Rak´ah thelathini na tisa. Kuna maoni ya wenye kusema ni Rak´ah ishirini na tisa. Kuna maoni ya wenye kusema ni Rak´ah ishirini na tatu. Kuna maoni ya wenye kusema ni Rak´ah kumi na tisa. Kuna maoni ya wenye kusema ni Rak´ah kumi na tatu. Kuna maoni ya wenye kusema ni Rak´ah kumi na moja. Yapo maoni mengine vilevile. Maoni yenye nguvu katika haya yote ni kwamba ni Rak´ah kumi na moja na kumi na tatu. Hayo ni kutokana na yale aliyopokea al-Bukhaariy na Muslim waliopokea kupitia kwa ´Aiashah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye aliulizwa ni vipi ilikuwa swalah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Ramadhaan ambapo akajibu:

“Hakuwa akizidisha katika Ramadhaan wala kwenginepo Rak´ah kumi na moja.”

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Swalah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) usiku ilikuwa Rak´ah kumi na tatu.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Maalik amepokea katika “al-Muwattwa´” kupitia kwa as-Saa-ib bin Yaziyd (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia:

“´Umar bin al-Khattwaab alimwamrisha ´Ubay bin Ka´b na Tamiym ad-Daariy wawaswalishe watu Rak´ah kumi na moja.”[1]

as-Salaf as-Swaalih walikuwa wakiirefusha sana. as-Saa-ib bin Yaziyd (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Msomaji alikuwa akisoma mamia ya Aayah mpaka tulikuwa tukiegemea bakora kutokana na urefu wa kisimamo.”

Hali hii ni tofauti na yale yanayofanywa na watu wengi hii leo ambapo wanaswali Tarawiyh kwa spidi kubwa na hawatekelezi utulivu ambao ni wajibu ambao ni nguzo miongoni mwa nguzo za swalah ambapo swalah haisihi isipokuwa kwa utulivu huo. Hivyo wanaharibu nguzo hii na wanawachokesha walionyuma yao katika wanyonge, wagonjwa na wazee. Wanazifanyia vibaya nafsi zao wenyewe na wanawafanyia vibaya wengine vilevile.

Wanachuoni (Rahimahumu Allaah) wamesema kuwa imechukizwa kwa imamu kuswali kwa haraka spidi ambayo itawakosesha waswaliji kufanya kile kilichosuniwa. Tusemeje juu ya spidi itayowakosesha kufanya kile ambacho ni wajibu? Tunamuomba Allaah usalama.

Haitakikani kwa mwanamme kuacha swalah ya Tarawiyh ili aweze kupata thawabu na ujira wake. Vilevile asiondoke mpaka imamu amalize kuiswali pamoja na Witr ili apate thawabu za kusimama usiku mzima.

[1] Ameipokea Maalik katika ”al-Muwattwa´” yake kwa cheni ya wapokezi ambayo ni Swahiyh zaidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 15/04/2020