21. Maana ya sifa za Allaah inajulikana na namna haijulikani

Hakuna yeyote anayejua namna sifa Zake zilivyo isipokuwa Yeye peke yake (Subhaanahu wa Ta´ala). Anajua tofauti na tunavyojua, anahurumia tofauti na tunavyohurumia, amelingana tofauti na tunavyolingana, hushuka tofauti na tunavyoshuka, huja tofauti na tunavyokuja na hughadhibika tofauti na tunavyoghadhibika. Vivyo hivyo inahusiana na sifa nyenginezo zote:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

Kulingana kunajulikana, huruma unajulikana, kughadhibika kunajulikana, kupenda kunajulikana na kutaka kunajulikana, utashi unajulikana. Ama kuhusu namna yake haijulikani. Hatujui namna alivyolingana. Hatujui namna anavyohurumia. Hatujui yote haya. Allaah Pekee ndiye mwenye kujua haya (Subhaanahu wa Ta´ala). Lakini hata hivyo tunajua kuwa kupenda sio kuchukia, kukasirika sio kuridhia, kuridhia sio kusamehe na kadhalika. Maana ya sifa inajulikana. Lakini haya hivyo namna yake hakuna mwenye kuijua isipokuwa Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kughadhibika kunajulikana ambako ni kinyume na kuridhia, kupenda ni kinyume na kukasirika, huruma ni kinyume na kupatiliza. Allaah anasifa nazo. Allaah huwahurumia baadhi ya watu na akawaadhibu wengine na wengine akawapatiliza. Huwahurumia watu wenye kupigana katika njia Yake na wengine akawaghadhikia na kuwapatiliza kwa kumuasi na kumkufuru. Hali ni namna hii ambapo Allaah anawapenda baadhi ya watu na wengine anawachukia, anawapa baadhi na wengine anawanyima. Yeye ndiye mwenye kuzuia na kutoa (Jalla wa ´Alaa). Huu ndio mfumo wa Ahl-us-Sunnah. Wanaziamini sifa na wakati huo huo wanaamini kuwa ni haki na kwamba zinalingana na Allaah na kwamba maana yake ni haki. Lakini hakuna anayejua namna yake isipokuwa Yeye Mwenyewe (Subhaanahu wa Ta´ala).

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com