20. Swalah ya usiku katika Ramadhaan ina sifa ya kipekee


Swalah ya usiku katika Ramadhaan ina fadhilah na sifa mbalimbali kuliko swalah nyenginezo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule atakayesimama kuswali Ramadhaan hali ya kuwa na imani na matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Maana ya maneno yake:

“… hali ya kuwa na imani.”

ni kumwamini Allaah na zile thawabu alizowaandalia wenye kufanya hivo. Maana ya maneno yake:

“… matarajio.”

akitafuta thawabu za Allaah na si kujionyesha, kutaka kusikika, kutafuta mali au cheo ndio kumempelekea kufanya hivo.

Kusimama kuswali Ramadhaan kunahusu kuswali sehemu ya mwanzo ya usiku na sehemu ya mwisho wake. Kujengea juu ya haya Tarawiyh ni katika kusimama kuswali Ramadhaan. Kwa hiyo inatakikana kwa watu kuipupia na kuitilia umuhimu na pia kutarajia malipo na thawabu kutoka kwa Allaah juu yake. Si vyenginevyo isipokuwa ni nyusiku zenye kuhesabika ambazo muumini mwenye busara anazitumia vyema kabla hazijamalizika. Imeitwa “Tarawiyh” kwa sababu watu walikuwa wakiirefusha sana. Kila wanaposwali Rak´ah nne wanapumzika kidogo.

Mara ya kwanza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisunisha kuswali Tarawiyh mkusanyiko msikitini. Kisha akaiacha kwa kuchelea isije kufaradhishwa kwa Ummah wake. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) usiku mmoja aliswali msikitini na akawaswalisha watu. Usiku wa kufuata akafanya hivo tena ambapo watu wakawa wengi. Usiku wa tatu wakakusanyika au wa nne lakini hata hivyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakujitokeleza kwao. Kulipopambazuka akasema:

“Nimeona kile mlichokifanya. Hakuna kilichonizuia kujitokeza kwenu isipokuwa mimi nilichelea isifaradhishwe kwenu.” ´Aaishah anasema: “Hapo ilikuwa katika Ramadhaan.”

Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Tulifunga pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hakusimama kuswali na sisi mpaka kulipobaki subui ya mwezi. Akasimama kutuswalisha mpaka ikaenda theluthi ya usiku. Hakusimama kuswali na sisi katika sudusi. Kisha akasimama kuswali na sisi katika humusi mpaka ikaondoka nusu ya usiku. Tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Lau ungetuswalisha usiku wetu huu uliobaki.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika yule atakayesimama pamoja na imamu mpaka akaondoka, basi ataandikiwa ameswali usiku mzima… “

Wamipokea watunzi wa Sunna kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 28-29
  • Imechapishwa: 15/04/2020